Home Habari za michezo USIYOYAJUA KUHUSU MKATABA MPYA WA SIMBA NA JAYRUTTY

USIYOYAJUA KUHUSU MKATABA MPYA WA SIMBA NA JAYRUTTY

Habari za Simba leo

KAMPUNI ya Jayrutty Investment Limited imeahidi kuijenga klabu ya Simba Uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 10,000.

Ahadi hiyo imetolewa na Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira baada ya Kampuni yake kutambulishwa ndiyo mshindi wa Tenda ya Usambazaji jezi za klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Sh. Bilioni 38.1 (Sh. 8,120,400,000).

“Jambo la kwanza ambalo tunakwenda kutekeleza ni kujenga Uwanja wa mpira, Uwanja ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000 na tumekubaliana kwamba Simba wana Uwanja Bunju na tutakwenda kujenga Uwanja Bunju, lakini kama watakuja na mapendekezo mengine basi tutayafuata,” amesema CPA Joseph Rwegasira.

Pamoja na hayo, CPA Joseph Rwegasira watainunulia Simba basi jipya aina ya Irizar, ambalo litaonekana hivi karibuni huku pia akisema watajenga chombo kikubwa cha habari kitakachokwenda sambamba na vymbo vya klabu nyingine kubwa.

“Tunajua kwamba Simba makao makuu yapo Msimbazi lakini tunakwenda kujenga ofisi za kisasa. Lakini pia kila mwaka tutatoa Tsh. 100 milioni ya kusaidia kukuza soka la vijana. Kila mwaka pia tutachangia Tsh. 100 milioni kuchangilia pre season,” amesema CPA Joseph Rwegasira na kuongeza;

“Pia tumeahidi kujenga kituo maalumu cha matibabu ya wachezaji. Kila mwaka pia tutashiriki bega bega katika Simba Day, tutachangia Tsh. 100 milioni kila mwaka.”.

Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ameipongeza Simba na Jayrutty Investment Limited kwa ndoa yao ambayo inaelekea kuleta mageuzi makubwa kwenye klabu hiyo.

“Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu imewekeza sana kwenye michezo na hasa mchezo huu pendwa wa mpira wa miguu. Ki takwimu hakuna kipindi tumefanya vizuri kama kipindi hiki.

Mchezo huu unaendelea kutupa raha mioyoni na kututangaza nje ya mipaka ya nchi,” amesema Mwinjuma maarufu kama Mwana FA.

“Hili nililosikia leo la ujenzi wa uwanja limenivutia sana. Mkiwa na kiwanja cha watu 10,000 au 12,000 kinaweza kutumika kwa michezo ya ndani, michezo ya nje ndio mkawa mnatumia Uwanja wa Mkapa, mtaupunguzia hata majukumu.”

“Itoshe kusema ni uwekezaji wa mkakati ambao umekuja wakati sahihi. Serikali kama mlezi wetu tunawapongeza sana. Naamini mna maarifa ya kucheza mchezo wa nusu fainali utakaochezwa Zanzibar na kule Afrika Kusini na kuhakikisha mnavuka na kuingia fainali hadi kushinda ubingwa wa Afrika,”.

“Na sisi kama serikali kama mara zote ambavyo tunawaunga mkono hatutawaacha hata wakati huu. Tupo nyuma yenu kuhakikisha mnashinda ubingwa wa Afrika. Hatuishii Hapa,” amesema Mwana FA.

Mapema akiitangaza Kampuni ya Jayrutty Investment Limited kuwa mshindi wa Tenda hiyo katika hafla iliyofanyika jioni ya leo Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Tenda, Simba SC, Dkt. Seif Muba amesema kwamba walipokea barua nyingi za maombi, lakini bodi ikaamua makampuni yashindane kwa tenda.

“Kampuni nane zilichukua tender document lakini kampuni sita zilirudisha document. Maombi ya wazabuni yalifunguliwa kwa uwazi na baada ya mchakato wazabuni wote walijulishwa mzabuni ambaye ameibuka mshindi kwa kuweka fedha na vitu vingi ambavyo tulihitaji. Tuliingia mkataba wa miaka mitano na kampuni hiyo,” amesema Muba na kuongeza;

“Mshindi aliyeshinda tenda hiyo ameshinda kwa kuweka kiasi cha fedha cha Tsh. 38 Bilioni. Napenda kuitangaza kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited kama mshindi. Klabu ya Simba inakwenda kupata Tsh. 5.6 Bilioni kwa mwaka.”

Kuhusu utekelezaji wa mkataba wake wa miaka mitano, CPA Joseph Rwegasira amesema pamoja na kutoa Sh. Bilioni 38 kwa mwka, pia watasajili mchezaji mmoja kila msimu ambaye atatakiwa na wana Simba.

“Hizi ni baadhi ya faida za ziada ambazo sisi tutatoa kwa Simba Sports Club. Kila mwaka tumekubali kutoa Tsh. 470 milioni kwa wachezaji, uongozi utagawa kwa namna ambayo wataona inafaa na hii fedha itakuwa inaongezeka kila mwaka.”

Aidha, CPA Rwegasira amesema kwamba wamekubali kutoa Sh. Milioni 470 kwa wachezaji, kila mwaka ambazo uongozi utazigawa kwa namna ambayo wataona inafaa na kwamba kutakuwa na ongezeko la fedha hizo kila mwakaa.

“Tumeingia mkataba wa kimataifa na brand mojawapo kubwa duniani ambayo inazivisha klabu nyingi kubwa. Mwaka huu na miaka inayofata mambo yatakuwa mazuri sana, tunakuja kuonyesha tofauti. Tutahakikisha Simba inapata thamani kubwa kulingana na ukubwa wake ndio maana tumewekeza fedha nyingi sana kwenye hili,”.

“Kwa mara ya kwanza Simba Sports Club itakuwa klabu ya kwanza Tanzania kuvaa jezi ambayo ni internationa brand. Naomba kuwambia kuanzia sasa mtakuwa na furaha isiyo na kifani. Kwa ushirikiano tulionao na uongozi tutahakikisha Simba inarudisha heshima yake sio tu nchini, Afrika na duniani. Nawashukuru sana Simba kwa kutuamini.”

“Hivi karibuni tutaitangaza brand ambayo itavalisha jezi. Tutapata ubora wa hali ya juu katika bei rafiki kabisa, kama Mwanasimba jivunie, kama uliweza kununua jezi zilizopita basi hata hivi utaweza. Nitoe pongezi kwa wazabuni waliopita, nitoe pongezi kwa Vunja Bei, nitoe shukrani kwa Sandaland na kubwa tuendelee kushirikiana,” amesema Rwegasira na kuongeza;

“Kiasi ambacho kimetajwa ni kiasi ambacho tumezingatia mambo mengi kama klabu. Nipende kuwahakikishia kabla hata hatujafanya kitu chochote tumeshaweka asilimia 30 ya hiki kiasi cha mwaka wa kwanza,” amesema Rwegasira.

Naye Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Ally Mangungu amewapongeza Wajumbe wa Kamati ya tenda iliyoundwa na Wenyeviti wa kamati ndogo za bodi.

“Mimi nawapongeza sana wajumbe hawa kwa kazi kubwa waliyofanya kwa niaba ya bodi. Bodi nzima iliridhia kwamba hakuna sababu aliyeshinda kutokupewa hii tenda. Mapinduzi makubwa ya jezi yalifanywa na Kassim Dewji kwa zaidi ya miaka 10,”.

“Miaka hiyo tulikuwa tunaletewa tu jezi nyeupe na nyekundu lakini yeye akaleta jambo la tofauti lakini game changer ni Vunja Bei yeye ndio akuja kuonyesha njia, Sandaland alifanya kazi yake lakini sasa amekuja Jayrutty,”

“Umeahidi mambo mengi uyafanyia kazi usijesema kwamba ulitamani brand kubwa lakini imeshindakana. Nawahakikishia Wanasimba wote tutashirikiana kufanikisha hilo. Tutashirikiana na mpango wa mwekezaji Mohammed Dewji hivyo hakutakuwa na kuingiliana katika utekelezaji wake,” amesema Manungu.

SOMA NA HII  NTIBAZONKIZA AVUNJA UKIMYA YANGA...ADAI ANA DENI ZITO...AMTAJA MAYELE NA NABI...