MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji, amewataka mashabiki wa timu hiyo kusitisha lawama kwa wachezaji na badala yake kuwaunga mkono katika kipindi hiki muhimu.
Akizungumza baada ya mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch FC uliochezwa Aprili 20 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar – ambapo Simba ilishinda bao 1-0 – Mo Dewji alisisitiza kuwa huu si wakati wa kulaumiana, bali ni muda wa mshikamano.
Kauli yake imekuja kufuatia mashabiki kumlalamikia beki Jean Charles Ahoua kwa kukosa bao la wazi katika mchezo huo. Hata hivyo, Mo Dewji amewatetea wachezaji akisema kuwa makosa ni sehemu ya mpira wa miguu.
“Kwa kosa moja lililotokea, hatuwezi kumsulubu mchezaji leo. Tukumbuke hata mastaa wa dunia kama Fernando Torres waliwahi kukosa mabao ya wazi kwenye mechi kubwa kama ya Chelsea dhidi ya Manchester United,” amesema.
Ameongeza kuwa Ahoua ni miongoni mwa wachezaji waliowapa mashabiki furaha msimu huu, na amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Simba.
“Hii ni soka – makosa ni ya kawaida, lakini jambo kubwa zaidi ni namna timu inavyosimama tena baada ya changamoto.
Tunajifunza, tunaimarika na tunapambana. Safari haijaisha. Mchezo wetu wa marudiano bado uko mbele,” amesisitiza Mo Dewji.
Mo ametoa wito kwa wanasimba wote kuungana, kuwa imara na kuendelea kuisapoti timu: “Simba inajengwa juu ya mshikamano. Tunasimama na Jean (Ahoua) na kila mchezaji anayejitoa kwa jezi ya Simba.”
Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka nchini hivi karibuni kwa ndege ya kukodi kuelekea Durban, Afrika Kusini, kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Stellenbosch FC, ambao utaamua hatma ya timu hiyo katika kampeni ya Kombe la Shirikisho Afrika.