Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA FAINAL YA CAF….HII HAPA AHADI YA ‘KISHUA’ YA RAIS...

KUELEKEA MECHI YA FAINAL YA CAF….HII HAPA AHADI YA ‘KISHUA’ YA RAIS SAMIA KWA SIMBA…

Habari za Simba leo

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameongeza zawadi ya fedha kwa klabu ya Simba SC kupitia mpango wa “Goli la Mama”, sasa wachezaji watapokea Shilingi milioni 30 kwa kila bao watakalofunga katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Awali, Rais Samia alikuwa ameahidi Shilingi milioni 20 kwa kila goli katika mechi za nusu fainali. Sasa, kutokana na hatua ya Simba kufuzu fainali, dau hilo limeongezwa kama sehemu ya hamasa kwa wachezaji kuhakikisha wanapambana ipasavyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amethibitisha taarifa hiyo akisema: “Rais anawatakia kila la kheri Simba katika hatua ya fainali na anaamini timu hiyo itabeba Kombe la Shirikisho Afrika. Katika mechi za fainali, kila bao moja litalipwa Shilingi milioni 30.”

Simba SC wanatarajiwa kukutana na RS Berkane ya Morocco katika fainali hiyo, ambapo mchezo wa kwanza utafanyika Mei 17 nchini Morocco, huku marudiano yakifanyika Mei 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Msigwa ameongeza kuwa iwapo Simba watafunga mabao mawili katika mechi, watalipwa Shilingi milioni 60, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa hamasa zaidi wachezaji, kuongeza morali, na kuhakikisha wanapeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.

SOMA NA HII  AZAM FC KAMILI GADO KUWAVAA PYRAMID YA MISRI