Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA FAINAL YA CAF J/PILI HII….CHE MALONE ‘AJIPA UMUHIMU’...

KUELEKEA MECHI YA FAINAL YA CAF J/PILI HII….CHE MALONE ‘AJIPA UMUHIMU’ SIMBA….

Habari za Simba leo

BEKI wa kati wa Simba SC, Che Malone Fondoh, ameweka bayana dhamira ya kikosi chao kubadilisha matokeo ya mchezo wa kwanza dhidi ya RS Berkane na kuandika historia mpya katika mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba watakuwa wenyeji wa Berkane katika uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Jumapili Mei 25, wakihitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Morocco, Simba walikubali kichapo cha mabao 2-0, lakini Che Malone anaamini kuwa hali inaweza kubadilika.

Beki huyo amesema mchezo huu una umuhimu wa kipekee kwake binafsi, kwani ni sehemu ya malengo yake ya kucheza na kushinda fainali za mashindano makubwa barani Afrika.

“Hii kwangu ni nafasi adhimu. Tulicheza kule Morocco, lakini hatukuwa katika ubora wetu. Tunajua nini tunatakiwa kufanya na tuna nafasi ya kubadilisha hali hiyo. inategemea maandalizi yetu, mtazamo wetu hata kwenye mazoezi. Kila mchezaji yupo tayari, tumekaa sawa kiakili na kimwili kwa ajili ya pambano hili,” amesema Che Malone.

Ameongeza kuwa huu ni miongoni mwa misimu bora kwake tangu aanze kucheza soka la kulipwa, na kutwaa ubingwa wa kombe hilo kutafanya msimu huu kuwa wa kipekee zaidi.

“Bado hatujakamilisha kazi, lakini tuna nafasi. Tukifanikiwa kuchukua ubingwa, basi huu utakuwa msimu bora zaidi kwa timu yetu na kwa kila mmoja binafsi. Tutapambana hadi dakika ya mwisho,” amesema.

Mashabiki wa Simba wana matumaini makubwa kuwa timu yao itaonesha uwezo mkubwa nyumbani na kuandika historia kwa kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, licha ya changamoto iliyo mbele yao.

SOMA NA HII  HII HAPA TAREHE MPYA YA MECHI YA DABI....MWEZI NI ULE ULE WA KICHEKO KWA YANGA....