Home Habari za michezo PAMOJA NA KUPATA UBINGWA WA FA JANA…NEEMA YAZIDI KUTUA YANGA…

PAMOJA NA KUPATA UBINGWA WA FA JANA…NEEMA YAZIDI KUTUA YANGA…

Habari za Yanga leo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ameizawadia Klabu ya Yanga shilingi milioni 100, kwa kutambua ushindi na mafanikio makubwa waliopata katika msimu wa mwaka 2024/2025.

Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Juni 30, 2025 alipokutana na viongozi pamoja na wachezaji wa Yanga waliofika Ikulu kwa ajili ya kumkabidhi makombe matano ya michuano mbalimbali waliyoyatwaa msimu huu.

Akizungumza nao, Dk Mwinyi amepongeza mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana na klabu hiyo kongwe, akieleza kuwa yanajenga heshima na historia muhimu katika tasnia ya michezo nchini.

Aidha, ameishukuru Yanga kwa kuendelea kuitangaza Zanzibar ndani na nje ya nchi kupitia kampeni ya Visit Zanzibar, huku akieleza kuwa hatua ya klabu hiyo kucheza baadhi ya michezo yake Zanzibar kunachangia kukuza uchumi na sekta ya utalii kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wageni na wananchi kunufaika na fursa mbalimbali.

Halikadhalika, Rais Dk Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha viwanja vya michezo ili kuwezesha michuano mingi zaidi kufanyika Zanzibar.

Rais wa Yanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vilabu vya Soka Barani Afrika, Mhandisi Hersi Said, amemkabidhi Rais Dk Mwinyi medali maalum ya Michuano ya CRDB pamoja na jezi ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League) pamoja na kutoa pongezi na shukrani kwa Rais Dk Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya michezo nchini na kuahidi kuwa klabu hiyo itaendelea kucheza mechi zake Visiwani.

Msimu huu, klabu hiyo imefanikiwa kutwaa makombe yafuatayo: Ngao ya Jamii ya Ligi ya NBC, Kombe la Michuano ya Toyota, Kombe la Muungano, Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara, na Kombe la Shirikisho la CRDB.

SOMA NA HII  MASHABIKI SIMBA WACHANGANA KUNUNUA BASI JIPYA....