Home Habari za michezo WAKATI WAKIENDA ‘PRI SIZONI’….HII HAPA PRESHA MPYA YA SIMBA KWA MSIMU UJAO….

WAKATI WAKIENDA ‘PRI SIZONI’….HII HAPA PRESHA MPYA YA SIMBA KWA MSIMU UJAO….

Habari za Simba leo

KABLA ya kuanza msimu uliopita, Simba chini ya Kocha Fadlu Davids iliwaeleza bayana mashabiki na wapenzi wa klabu wasitarajie maajabu kwa timu hiyo kwa vile wanajenga kikosi.

Kauli hiyo ilitolewa na mabosi wa klabu hiyo akiwamo Ofisa Habari, Ahmed Ally na hata kocha Fadlu kutokana na ukweli, Simba ilifumua kikosi kwa kutema mastaa kibao hasa walioonekana kuwa na umri mkubwa na wale walioshindwa kuonyesha uwezo.

Simba iliwapiga chini kina John Bocco, Saido Ntibazonkiza, Luis Miquissone, Clatous Chama, Freddy Michael, Moses Phiri, Kennedy Juma, Henock Inonga, Saleh Karabaka, Mohamed Mussa, Willy Onana na Pa Omar Jobe.

Kisha ikaleta wachezaji wapya wenye umri mdogo, ambao walishtua mashabiki kwa vile wengi hawakuwa na majina makubwa kulinganisha na waliosajiliwa na timu nyingine kama Yanga, Azam, Singida Black Stars na Tabora United.

Ndipo ikaibuliwa hiyo slogan ya ‘Simba tunajenga timu’, ili kuwapunguzia presha Wanasimba, lakini cha ajabu timu ilifanya maajabu kwa kukomaa katika vita ya ubingwa jadi mwisho wa msimu.

Simba ilimaliza ya pili nyuma ya Yanga kwa tofauti na pointi nne tu, ikafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikapoteza kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-1.

Mashabiki wakajipiga kifua kwa kuamini kama msimu mmoja wa kikosi kujengwa chini ya Fadlu, timu imefika fainali ya CAF na kuichachafya Yanga ambayo misimu mitatu nyuma ilikuwa ikibebea ubingwa wa Ligi Kuu mapema ikiwa na mechi kadhaa mkononi.

Hata hivyo, ghafla mashabiki wa Simba wameshuhudia kikosi cha timu hiyo kikibomolewa tena kwa wachezaji tisa waliokuwa sehemu ya ‘ujenzi’ timu hiyo kwa msimu uliopita wakitemwa kwa kupewa ‘thank you’.

Aishi Manula, Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Hussein Abel, Fabrice Ngoma, Kelvin Kijili, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Valentin Nouma wamepewa thank you, huku Omar Omar akirudishwa Mashujaa kwa mkopo.

Inadaiwa wapo wachezaji wengine wapo njiani kutolewa Msimbazi ama kwa kuuza au kwa mkopo, ili kuruhusu mashine mpya ziingie kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.

PRESHA MPYA

Kutemwa karibu kikosi kizima kati ya wachezaji waliounda Simba ya msimu uliopita ina maana kocha Fadlu na mashabiki wanaanza presha mpya.

Ndiyo, Yanga, Azam, Singida BS zote zimeonyesha mapema zipo bize kuviimarisha vikosi vyao kwa kuviongezea watu wa maana. Hazijabomoa timu zilizokuwa nazo msimu uliopita na zilizotoa upinzani kwa Simba.

Kwa sababu Simba ni kama inaanza upya kusuka kikosi ilichokuwa nacho kwa maingizo mapya, ni kama walipiga hatua 10 mbele kisha kurudi 15 nyuma.

Licha ya kwamba kila kitu ni mipango, lakini kupanga si matumizi, ni ukweli ulio wazi Simba inaanza hesabu mpya na inategemea na wachezaji watakaosajiliwa watafanya kitu gani.

Hutokea wakati wachezaji wapya husajiliwa na kushika maelekezo ya makocha mapema na kuzibeba timu kama ilivyokuwa kwa kina Meddie Kagere, Luis Miquissone, Jean Baleke, Moses Phiri, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala na Saido Ntibazonkiza walipotua Msimbazi.

Lakini wapo wanaochukua muda kwenda na kasi au kuchemsha kabisa kama ilivyotokea kwa Boubacar Sarr, Pa Omar Jobe, Valentine Mashaka, Mohamed Mussa na wengine waliosajiliwa Msimbazi na baadae kuondolewa.

MCHANGO WA WALIOONDOKA

Ukiondoa kipa Aishi Manula ambaye msimu mzima hakucheza kabisa, sambamba na Omar Omar ambaye alicheza mechi moja akitokea benchi, nyota wengine waliotemwa Msimbazi wana sehemu ya mchango mkubwa kwa timu hiyo kwa msimu uliopita.

Kelvin Kijili ukiacha bao la kujifunga dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo ya Oktoba 19 mwaka jana, ni beki aliyekuwa akitumika japo kwa kutokea benchi kuimarisha eneo la ulinzi akimpokea mkongwe Shomary Kapombe. Sio beki wa kubezwa kwa dakika alizocheza, lakini ndo kaachwa na ameshatua Singida BS.

Fabrice Ngoma, moja ya sajili zilizosisimua Bongo, ni kiungo na mchezaji mzoefu aliyekuwa roho ya Simba tangu atue Msimbazi, alisaidia kuituliza Simba na kuifungia mabao muhimu msimu uliopita na kuiwezesha Simba kufika fainali ya Caf. Ameondoka akiwa ameifungia timu hiyo mabao manne katika Ligi Kuu Bara.

Mohammed Hussein, beki na mchezaji mwandamizi aliyemaliza mkataba Msimbazi baada ya kuitumikia kwa miaka 11 tangu 2014, ameondoka akiwa ameifungia bao moja na asisti nne, lakini akiwa sehemu ya mafanikio ya timu kwa msimu uliopita anga za kimataifa kwa aina yake ya uchezaji na kujituma akiwaongoza wenzake kama nahodha.

WENGINE

Debora, Nouma, Okejepha ni kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa msimu uliopita na hawakupata muda mrefu wa kutumika kwa presha iliyokuwapo ya Simba kuhitaji matokeo zaidi, lakini sio wachezaji wa kubezwa kwani dakika chache walizotumika na umri walionao walionyesha wana kitu ni vile tu, mambo hayakuwanyookea.

Kwa Hussein Kazi mambo yalikuwa magumu tangu ujio wa Abdulaziz Hamza na Chamou Karabou waliokuwa wakitumika zaidi sambamba na Fondoh Che Malone, lakini beki mzuri, wakati Omar alichemsha mapema pengine kutokana na watu waliokuwa katika eneo la kiungo analocheza ambalo liliwatibulia hadi kina Debora na Okejepha licha ya timu walizotoka walikuwa moto.

WASIKIE WADAU

Hata hivyo, wakizungumzia  juu ya fagia fagia hiyo, wakongwe wa soka waliowahi kuichezea Simba wamesema kinachofanyika kama ni mikakati ya benchi la ufundi hakuna anaeweza kuingilia lakini kama ni maamuzi ya watu binafsi wanaharibu timu.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel ‘Batgoal’ alisema ni kweli Simba walisema wanatengeneza timu lakini haina maana hawaruhusiwi kuvunja kama wachezaji walikuwa na matarajio tofauti na waliyoyaonyesha.

“Wachezaji sawa na ajira ya kocha tu unasajiliwa na unaweza kuachwa muda wowote kwa walichokifanya wanatakiwa kusajili nyota wenye uzoefu na ubora ili waweze kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza vinginevyo kila msimu watakuwa wanajenga timu mpya,” anasema na kuongeza;

“Timu inatwaa mataji lakini bado inaacha wachezaji sishangazwi na kinachofanywa na Simba timu nyingi zinafanya hivyo lengo ni kutengeneza timu yenye uwiano wa wachezaji wenye ubora, ukitazama nyota wengi waliachwa wakiwa bado wana mikataba walishindwa kuendana na kasi ya timu unabaki nao ili iweje,” alisema.

Kiungo na nahodha wa zamani wa Simba na Stars, Henry Joseph aliungana na Batgoal kwa kusema mabadiliko ya timu yapo na huwa yanafanyika mara nyingi huku akiweka wazi kunakuwepo na hata ambayo hayakutarajiwa.

“Pengine kuna vitu wameviona kutoka kwa wachezaji hao, hayo ni mabadiliko ya timu na sehemu yoyote yapo, Simba inataka mafanikio na kurudi kwenye ubora wao wa miaka kadhaa iliyopita hivyo ni lazima waondoe wale ambao wanaona kwa wakati huo hawahitaji kuendelea nao.

“Lakini wanatakiwa kuwa na machaguo mazuri ili kujiweka kwenye nafasi ya kudumu na wachezaji muda mrefu kama ilivyokuwa misimu minne nyuma ambayo walikuwa na mafanikio wakizingatia ubora na uzoefu kutokana na kuhitaji mafanikio ya haraka,” alisema Henry aliyewahi kukipiga Mtibwa.

SOMA NA HII  GAMONDI ATAMBA, YANGA BADO HAWAJAANZA KUTUMIA MIFUMO YAKE