Home CAF CHAN 2024: HIVI NDIVYO TANZANIA ILIVYOZIPIGA BAO KENYA, UGANDA….KAZI IKO HAPA….

CHAN 2024: HIVI NDIVYO TANZANIA ILIVYOZIPIGA BAO KENYA, UGANDA….KAZI IKO HAPA….

CHAN 2024

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeandika ukurasa mpya kwa ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kuanza kwa kishindo michuano ya CHAN 2024, huku ikizidi kete majirani zake Kenya na Uganda waliokuwa kama wenyeji wenza wa mashindano hayo.

Ilianza kwa kishindo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Jumamosi ya Agosti 2, wakati Stars ilipowatendea haki Watanzania kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi B, ikionyesha ubora mkubwa katika kila idara.

Mabao ya Abdul Suleiman ‘Sopu’ kwa njia ya penalti na la beki mkongwe Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ yaliipa Stars ushindi katika mechi hiyo, huku ikitawala kwa asilimia kubwa na kuwapa mashabiki wa Tanzania sababu ya kutabasamu.

Siku moja baadaye, ilikuwa ni zamu ya Kenya, waliokuwa wenyeji wa pili wa mashindano haya kwa wachezaji wa ndani. Waliikaribisha DR Congo mabingwa mara mbili wa CHAN katika Uwanja wa Moi, Nairobi.

Ingawa walikabiliwa na upinzani mkali, bao pekee la Austin Odhiambo dakika ya 45+2 liliwatosha kuibuka na ushindi wa 1-0, na kuamsha shangwe miongoni mwa maelfu ya mashabiki waliokuwepo uwanjani.

Hata hivyo, hali haikuwa nzuri kwa Uganda, ambao ni wenyeji wenza wa tatu wa michuano hii. Jumatatu ya Agosti 4, walikumbana na kipigo kizito cha mabao 3-0 kutoka kwa Algeria katika Uwanja wa Mandela, Kampala.

Licha ya sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao, Uganda walionekana kuzidiwa maarifa na kasi ya Waarabu hao.

Matokeo hayo yameiacha Uganda ikihitaji kufanya kazi ya ziada kwenye mechi zake tatu zilizosalia dhidi ya Guinea, Afrika Kusini, na Niger ili kufufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali.

Kwa upande mwingine, Stars na Kenya wameanza vizuri kampeni zao, na sasa wanahitaji kuendeleza kasi hiyo kwenye michi zao zinazofuata ili kutetea heshima ya ukanda huu wa Afrika Mashariki, ambao kwa mara ya kwanza katika historia unashikilia mashindano haya kwa pamoja.

Kocha wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, ameonekana kulijenga kikosi chenye nidhamu na umoja, huku wachezaji wakionekana kuelewa majukumu yao. Ushirikiano kati ya viungo na safu ya ushambuliaji ulionekana kuzaa matunda, huku mabeki wakicheza kwa umakini.

Kwa Kenya, ushindi dhidi ya DR Congo ulikuwa wa kihistoria, ukizingatia kwamba wapinzani wao wamewahi kutwaa ubingwa wa michuano hii mara mbili. Kwao, hilo lilikuwa jambo la kujivunia na kuwatia moyo kabla ya mechi zao zinazofuata dhidi ya Angola, Zambia na Morocco.

SOMA NA HII  KUMWEMBE AMVAA MAYELE ...AMPA MAKAVU LIVE..."UNATAKA KUONEKANA MFALME