Home Habari za michezo KUELEKEA KUANZA KWA MSIMU MPYA…HII HAPA KAULI YA ENG HERSI KWA YANGA…SIMBA...

KUELEKEA KUANZA KWA MSIMU MPYA…HII HAPA KAULI YA ENG HERSI KWA YANGA…SIMBA 😱😱..

Habari za Yanga leo

KLABU ya Yanga imesema imeridhishwa na kikosi chao cha msimu mpya ujao wa mashindano na kwamba ina matumaini makubwa ya kubakiza makombe yao yote iliyonayo na kufanya vema kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kuanza katikati ya mwezi ujao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said na makamu wake, Arafat Haji, walisema wameridhishwa pia na uwezo wa Kocha Mkuu mpya, Romain Folz raia wa Ufaransa, hivyo wataendelea kumpa muda wa kukinoa kikosi hicho ambacho kimevutia mashabiki wengi wa soka nchini Rwanda.

Ijumaa iliyopita, Yanga ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Rayon Sports, Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda, ikishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na Andy Boyeli, Pacome Zouzoua na Bakari Mwamnyeto huku wakiwapa bao wenyeji kwa kujifunga kupitia kwa Aziz Andambwile.

“Tulikuwa kwenye maandalizi, ni mapema kuiona timu ikiwa kwenye shepu yake iliyozoeleka lakini tumeridishwa na viwango vya wachezaji wetu wapya waliokuwepo na hata kocha wetu.

Mechi ile ya Ijumaa iliyopita ilikuwa ni sehemu ya maandalizi yetu, tumeitumia kuwachezesha kwa mara ya kwanza wachezaji wetu wapya, ilikuwa ni nzuri kwao ili kuingia taratibu kwenye kikosi, ugumu ulikuwa hapo, lakini tulibaki kwenye falsafa ya Yanga kuhitaji mafanikio kwenye kila mashindano tunayocheza, tunamshukuru Mungu tumepata matokeo,” alisema Hersi.

Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, aliwashukuru wenyeji wao kwa mapokezi mazuri, huku akilisifia Tamasha la Rayon Sports Day, kuwa lilifana sana.

Makamu wa rais, Arafat, alisema ameridhishwa na viwango vya wachezaji kwani licha ya kwamba ni mechi ya kwanza lakini wameonesha uwezo mkubwa ikiwa ni siku chache tu baada ya maandalizi ya msimu.

“Tumeridhishwa na viwango vya wachezaji wetu wote walioingia kipindi cha dirisha kubwa la usajili. Kocha mpya naye ametutia moyo, pamoja na wachezaji wote wa zamani.

“Malengo yetu yapo pale pale, ni kuchukua makombe yote, tufanye vizuri pia kwenye mechi za kimataifa.

“Wachezaji wetu wanajua ukubwa na nembo wanayoivaa, thamani ya timu wanayoichezea na maana ya klabu hii kushinda makombe yote,” alisema Arafat.

Kuhusu mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, alikataa kuizungumzia akisema wao wamejiandaa kucheza mashindano yote na si mechi moja tu.

“Tumeiandaa timu yetu kwa kucheza mashindano yote msimu huu, si kucheza na Simba tu, lakini pamoja na hayo tuko tayari kucheza na yeyote tutakayepangwa naye Ngao ya Jamii hata kama itakuwa si timu nne kama ilivyokuwa awali,” alisema.

Kikosi cha Yanga kimerejea jijini Dar es Salaam baada ya mchezo huo ambao wanachama na mashabiki wa timu hiyo waliwaona baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa kwa msimu ujao wa mashindano.

Wachezaji hao ni Boyeli, aliyepachika bao, Mohamed Doumbia, Moussa Balla Conte, Celestin Ecua, Offen Chikola na wengineo.

SOMA NA HII  YANGA, COASTAL UNION WATAMBA …LAZIMA TUWANYOOSHE