Home Habari za michezo KISA USHINDI KIDOGO JUZI….. PEDRO ACHEFUKWA YANGA….

KISA USHINDI KIDOGO JUZI….. PEDRO ACHEFUKWA YANGA….

914
0
Habari za Yanga leo

LICHA ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amewawakia mastaa wa timu hiyo hawakucheza katika ubora kutokana uchovu, ingawa alikiri walikutana na wapinzani ambao walikuwa na mkakati wa kujilinda.

Yanga ilipata ushindi kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi 13 na kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na sasa itasafiri hadi Dodoma ili kesho Jumapili kukabiliana na Coastal Union katika mechi nyingine ya Ligi Kuu itakayosimama hadi Januari 21 mwakani.

Akizungumza  baada ya mechi hiyo ya tano kwa Yanga katika ligi ya msimu huu, amesema matokeo waliyopata haikuwa kazi rahisi kutokana na Fountain walivyoingia na mkakati wa kujilinda zaidi na wachezaji wa Yanga kufanya kazi kubwa kuivuka ngome iliyokuwa na watu tisa.

“Haikuwa rahisi wapinzani wetu walikuwa na mkakati wa kuzuia zaidi, hivyo kufungua ngome yao ilitumika nguvu kubwa licha ya ukweli baadhi ya wachezaji wangu niliowapa nafasi kutokuwa bora, japo tumefanikiwa kupata ushindi huo mzuri kwetu,” amesema Pedro na kuongeza:

“Kikosi kilikuwa na mabadiliko, nilitoa nafasi kwa wengine ambao hawakuwa na wakati mzuri kupata nafasi mechi zilizopita, ila hawakuwa bora sana lakini wamefanya kazi. Naamini nina kibarua kuwajenga kuwa katika ubora sawa na wenzao wanaocheza mara kwa mara.”

Pedro amesema bado ana ratiba ngumu kutokana na kuwa na viporo vingi kwa ajili ya mechi za ndani, hivyo atalazimika kufanya mabadiliko ili kutoa nafasi ya mapumziko kwa wengine wanaotumika sana na hilo litakuwa endelevu.

“Pamoja na kutoona ubora uliotarajiwa licha ya kukutana na mpinzani aliyekuwa na mbinu ngumu, naamini nitafanyia kazi upungufu niliuona kabla ya kuikabili Coastal Union,’’ amesema.

“Tunakuwa na muda mchache wa kufanya mazoezi ya kurudisha utimamu wa mwili kabla ya kuvaana na wapinzani. Hili ndilo shina linalofanya wachezaji wanacheza chini ya kiwango, sitakiwi kujitetea kwa hili kwani nina wachezaji wengi kazi niliyo nayo ni kujenga uwezo sawa.”

PESA ZA DIARRA

Kocha huyo pia alizungumzia kitendo cha mashabiki wa timu hiyo kummwagia fedha kipa namba moja, Diarra Djigui kutokana na ubora aliouonyesha katika mechi iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie akisema ni jambo zuri la kuendelea kuboresha uwezo wa wachezaji na kutoa chachu ya ushindani.

“Nimefurahishwa na namna mashabiki walivyohamasika kumchangia mchezaji kiasi cha fedha kutokana na ubora. Hii itatoa chachu kwa wengine kuonyesha juhudi uwanjani, pia kwa Diarra mwenyewe kuendeleza ubora ni nzuri,” amesema Pedro na kuongeza:

“Hii kwa wachezaji inaongeza morali na pia ushindani wao kwa wao kila mmoja atataka kuibuka shujaa kwenye mchezo husika ili aweze kutuzwa kama ilivyo kwa Diarra. Imenifurahisha na naamini itanirahisishia kazi kwa kuongeza ubora kwa mchezaji mmoja mmoja.”

Pedro amesema mpira una wachezaji 12 na huyo mchezaji wa mwisho – 12 (shabiki) ili apate furaha anahitaji burudani kutoka kwa nyota 11 anaowaamini hivyo furaha ya mashabiki itategemea ubora wa wachezaji mmoja mmoja na pia timu kwa ujumla ambayo itatoa matokeo mazuri na mchezo mzuri uwanjani.

“Hii ni kubwa sana na wachezaji wanatakiwa kuipa thamani ukiondoa soka na kuitumikia Yanga ni ajira yao bado. Kuna watu nje ya uwanja wanategemea ubora wao ili wafurahie na ndio maana wanajitoa na wao wanatakiwa kujitoa kwa hali na mali ili kuipambania nembo ya timu.”