Home Habari za michezo KUELEKEA DIRISHA DOGO…USAJILI MPYA WA YANGA HUU HAPA….

KUELEKEA DIRISHA DOGO…USAJILI MPYA WA YANGA HUU HAPA….

22
0
Habari za Yanga leo

ILI kukiongezea nguvu kikosi chake, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema katika ripoti yake anahitaji wachezaji watatu wapya wasajiliwe kipindi cha dirisha dogo la usajili, huku winga wa Vipers na Timu ya Taifa ya Uganda (Cranes), Allan Okello, akihusishwa kutua mitaa ya Jangwani.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kocha huyo raia wa Ureno anahitaji kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na winga mmoja.

Chanzo chetu kinasema Pedro pia anapanga kuwahamisha baadhi ya wachezaji wake nafasi wanazocheza kwa sasa na kuhamia nyingine kutokana na kuonekana ni mahiri zaidi kuliko sehemu walizozoeleka.

Chanzo kilisema ripoti aliyowasilisha kocha huyo kwa viongozi inasisitiza wanahitaji kiungo mkabaji halisi ili amhamishe kiungo raia wa Kenya, Duke Abuya, acheze namba nane.

“Kocha anamtumia Duke kama namba sita, kiungo mkabaji, lakini anasema jamaa ana uwezo mkubwa sana kama atamsogeza juu kidogo na kumpunguzia majukumu ya kukaba moja kwa moja.

Anasema kama akisogea mbele itaifanya Yanga kuwa na ubora mkubwa eneo la katikati kutokana na uwezo wa Mkenya huyo sambamba na kiungo mpya watakayemsajili,” kilisema chanzo.

Aliongeza mbali na kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, Duke anaongoza kwa kutoa pasi nyingi za mabao katika kikosi cha Yanga na Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ujumla.

Ana ‘asisti’ tatu, sawa na winga wa Simba, Mkongomani, Elie Mpanzu na straika wa Namungo, Raymond Chamungu.

Taarifa zinasema Pedro anaona iwapo atasogea mbele kidogo atakuwa na uwezo mkubwa wa kuisaidia timu pamoja na kufunga mabao.

Kuhusiana na nafasi ya kiungo mshambuliaji, kwa sasa inadaiwa Pedro haridhishwi na nyota wanaocheza eneo hilo zaidi ya Pacome Zouzoua, lakini amebaini nyota huyo raia wa Ivory Coast ni mzuri zaidi akicheza akitokea pembeni kuliko akiwa namba 10.

“Kocha anasema anataka awe anamtumia Pacome akitokea pembeni kwa sababu kila anapomweka huko anakuwa hatari zaidi kwa wapinzani kuliko akicheza namba 10, ingawa anaimudu vizuri.

Anataka atafutiwe winga mmoja mwenye ubora ambaye atazalisha mashambulizi kutoka pembeni,” kilisema chanzo chetu na kumtaja tayari macho na nguvu za mabosi wa Yanga zinaelekea kwa Okello, ambaye alionyesha uwezo mzuri kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zilizofanyika Agosti, mwaka huu.

“Lengo la kwanza ni kumpata Okello na juhudi zimeanza, kama akikosekana basi tutamsaka mwingine,” aliweka wazi mtoa taarifa huyo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alikiri klabu tayari imepokea ripoti kutoka kwa Pedro, ingawa hakusema kilichokuwa ndani ya ripoti hiyo.

“Tayari Kocha Pedro amewasilisha ripoti ikitaja maeneo ambayo anahisi yanatakiwa yaboreshwe, amewasilisha pia majina ya wachezaji ambao anaamini wanaweza kuisaidia Yanga.

Kama tulivyosema tutafanya usajili mapema zaidi kukimbizana na muda, tunataka kukimsajili mchezaji acheze mechi inayofuata dhidi ya Al Ahly ya Misri, siyo kusubiri taratibu, sijui vibali, kama yupo anasajiliwa moja kwa moja anakwenda kwenye mazoezi,” alisema Kamwe.

Aliongeza viongozi wamejipanga kupambana kuhakikisha wanapata wachezaji ambao wataleta ushindani ndani ya kikosi chao.

“Dirisha la usajili kipindi hichi huwa ni gumu kwa sababu wachezaji wengi wazuri wanakuwa bado hawajamaliza mikataba yao. Malengo yetu ni kuona tunatetea makombe yote na kuwataka mashabiki wawe watulivu kipindi hiki wanachokwenda kufanya usajili wa dirisha dogo, sisi huwa hatukosei kwenye usajili tupo makini mno,” Kamwe alitamba.

Yanga ambao wako hatua ya makundi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la FA.