Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, ameeleza kuwa klabu hiyo inaendelea na mipango yake ya ujenzi wa uwanja wa kisasa eneo la Jangwani bila makelele, hatua zilizofikiwa mpaka sasa zipo katika mwelekeo mzuri.
Rais huyo amesema mpango wa uwanja huo ni sehemu ya ahadi aliyoitoa rasmi mbele ya Wanachama katika Mkutano Mkuu wa klabu, kuwa suala hilo limepewa kipaumbele kikubwa ndani ya uongozi wake.
Hersi amesema amekuwa akitoa nafasi kwa Wanachama kumuuliza na kupata ufafanuzi kuhusu maendeleo ya uwanja huo, jambo linaloonyesha uwazi na uwajibikaji wa uongozi wa sasa wa Yanga katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
“Niliahidi na nitatekeleza. Siwezi kusema jambo kisha nishindwe kulitimiza,” amesena na ameonyesha msimamo wake kuwa ahadi ni deni, hasa kwa klabu kubwa yenye historia na matarajio makubwa kama Yanga.
Amesisitiza kuwa falsafa ya uongozi wake si kupiga kelele bali kufanya kazi kimya kimya na kuonyesha matokeo, kuwa Yanga inaongozwa kwa mipango madhubuti yenye malengo ya muda mfupi na mrefu.
Kauli hiyo imeendelea kuwapa matumaini makubwa Wanachama na mashabiki wa Yanga, ambao kwa sasa wanaamini kuwa ndoto ya kuwa na uwanja wao binafsi Jangwani ipo njiani kutimia chini ya uongozi unaothamini ahadi na utekelezaji.