UONGOZI wa klabu ya Simba umeendelea kuimarisha benchi la ufundi kwa kumtambulisha rasmi mchambuzi wa video, Prinil Deen, hatua inayolenga kuongeza ubora wa maandalizi na ushindani wa timu katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Kupitia taarifa rasmi, Simba imeeleza kuwa ujio wa Prinil Deen ambaye aliwahi kupita klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ni sehemu ya mkakati wa klabu kuendana na mahitaji ya soka la kisasa linalotumia teknolojia katika kuchambua michezo, wapinzani na maendeleo ya wachezaji.
Prinil Deen anatarajiwa kuwa na jukumu kubwa la kuchambua mechi za Simba pamoja na wapinzani wao, huku akitoa taarifa za kiufundi zitakazosaidia benchi la ufundi kupanga mbinu bora kabla na baada ya kila mchezo.
Uongozi wa Simba umeeleza kuwa uwepo wa mchambuzi wa video utaongeza ufanisi katika utendaji wa timu, hasa katika kurekebisha makosa, kuboresha mifumo ya uchezaji na kuongeza ushindani wa ndani kwa ndani miongoni mwa wachezaji.
Hatua hii ya Simba kumtambulisha mchambuzi wa video inaonesha dhamira ya dhati ya klabu hiyo kuwekeza katika taaluma na teknolojia, ikiwa ni sehemu ya safari ya kuhakikisha inabaki kuwa miongoni mwa klabu bora na zenye ushindani mkubwa Afrika.