Home Habari za michezo SIMPARA NA BASADIEN KUIMARISHA ULINZI MSIMBAZI

SIMPARA NA BASADIEN KUIMARISHA ULINZI MSIMBAZI

62
0

UONGOZI wa klabu ya Simba SC upo katika mchakato wa kuimarisha safu yake ya ulinzi kuelekea dirisha la usajili, huku majina mawili yakitajwa kuingia kwenye rada za Wekundu wa Msimbazi.

Mabeki hao ni Ismaila Simpara wa Stade Malien pamoja na Fawaaz Basadien anayeichezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa Simba wanaendelea kufanya tathmini ya kina juu ya uwezo wa mabeki hao wawili, lengo likiwa ni kumpata angalau mmoja wao ili kuongeza uimara na ushindani katika safu ya nyuma ya kikosi hicho msimu huu.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, mchakato huo unahusisha ufuatiliaji wa mechi mbalimbali walizocheza wachezaji hao pamoja na kufanya uchambuzi wa kiufundi ili kuona nani atakayefaa zaidi kuendana na falsafa ya benchi la ufundi la Simba.

Imeelezwa kuwa pendekezo la kumnasa beki wa Mamelodi Sundowns, Fawaaz Basadien, kwa mkopo limetolewa na kocha mpya wa Simba, Steve Barker, ambaye anaifahamu vizuri soka la Afrika Kusini na uwezo wa mchezaji huyo.

“Mchakato wa usajili unaendelea kwa kuzingatia mahitaji yaliyobainishwa na benchi la ufundi. Ripoti inaonyesha wazi kuwa tunahitaji kuimarisha safu ya ulinzi,” kimenukuliwa chanzo hicho kikisema.

Chanzo hicho kimeongeza kuwa tayari kocha Barker amekabidhiwa ripoti ya tathmini baada ya kuangalia mechi kadhaa za Simba msimu huu, hatua iliyomsaidia kubaini maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maboresho kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho ya usajili.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, aliwahi kuweka wazi kuwa baada ya kumpata kocha huyo mpya, uongozi ulimkabidhi ripoti ya kikosi ili aipitie na kushirikiana na benchi la ufundi katika kufanya usajili utakaokiimarisha kikosi cha timu hiyo kulingana na malengo ya klabu.