Home Habari za michezo MZIZI WA FITNA NA WAPINZANI WAVUNJWA NA MPANZU

MZIZI WA FITNA NA WAPINZANI WAVUNJWA NA MPANZU

18
0

LICHA  ya tetesi nyingi zilizokuwa zikimzunguka kila dirisha la usajili, hatimaye kiungo Elie Mpanzu ametua na kujiunga na kikosi cha Simba kilichopo kambini Visiwani Zanzibar, hatua iliyowavunja matumaini waliodai hatorejea tena ndani ya Wekundu wa Msimbazi.

Kwa kipindi kirefu, jina la Mpanzu limekuwa likitajwa kuhusishwa na uwezekano wa kujiunga na Yanga, huku madai yakizidi kushika kasi kutokana na mkataba wake kubakiwa na muda wa miezi sita pekee. Hali hiyo ilizua sintofahamu kubwa miongoni mwa mashabiki wa Simba kuhusu mustakabali wa nyota huyo.

Hata hivyo, kurejea kwake kambini kumeonyesha msimamo tofauti, ambapo Mpanzu ameonesha dhamira ya kuendelea kuitumikia Simba na kupambana kwa ajili ya mafanikio ya timu hiyo katika michuano inayoendelea.

Nyota huyo aliwasili Zanzibar na kuungana moja kwa moja na kikosi, huku akionekana kuwa sehemu ya wachezaji waliokuwepo jukwaani jana usiku kushuhudia timu yake ikiibuka na ushindi dhidi ya Muembe Makumbi City katika Kombe la Mapinduzi.

Uwepo wake kambini umeongeza morali kwa wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi, hasa ikizingatiwa uzoefu na mchango wake mkubwa katika kikosi cha Simba.

Mpanzu anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani katika mchezo ujao wa michuano hiyo dhidi ya Fufuni SC, unaotarajiwa kuchezwa kesho Jumatatu Januari 5, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kwa kurejea kwake, Mpanzu ameweka wazi kuwa bado ni sehemu ya Simba, akifunga mjadala uliokuwa unaendelea na kuwaacha mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona mchango wake ndani ya uwanja katika michezo ijayo.