KIKOSI cha Yanga kimeendelea kudhihirisha ubora wake baada ya kuanza kwa kishindo mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya KVZ katika mchezo uliochezwa kwa ushindani mkubwa visiwani Zanzibar.
Yanga ilianza mchezo kwa kasi na dhamira ya wazi ya kutafuta ushindi wa mapema, hali iliyowalazimu KVZ kujilinda kwa muda mrefu katika eneo lao. Shinikizo hilo liliwapa Wananchi matokeo dakika ya 32, pale kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua alipofunga bao la kwanza baada ya kumalizia kwa ustadi krosi safi kutoka kwa Max Nzengeli.
Baada ya bao hilo, Yanga iliendelea kutawala mchezo kwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga. KVZ walijaribu kujipanga upya kwa kujilinda kwa nidhamu na kusubiri mashambulizi ya kushtukiza, lakini hawakufanikiwa kubadili mwelekeo wa mchezo. Kipindi cha kwanza kilimalizika Yanga wakiwa mbele kwa bao 1-0, licha ya Nzengeli kukosa nafasi nzuri dakika ya 45 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango.
Kipindi cha pili Yanga walirejea uwanjani wakiwa na kasi zaidi, wakiongeza presha iliyowavuruga mabeki wa KVZ. Mashambulizi hayo yaliwazaa matunda dakika ya 55, ambapo Célestin Ecua alifunga bao la pili na kuzidisha maumivu kwa wapinzani wao.
Bao hilo liliwakatisha tamaa KVZ na kuwapa nguvu zaidi Wananchi kuendelea kushambulia. Yanga waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao kwa mashambulizi ya kasi kutoka pembeni pamoja na pasi za haraka katikati ya uwanja, wakionyesha tofauti kubwa ya kiwango kati ya timu hizo mbili.
Hatimaye, Yanga walihitimisha ushindi wao kwa bao la tatu lililotokana na makosa ya ulinzi wa KVZ, hali iliyompa nafasi Emmanuel Mwanengo kutikisa nyavu. Ushindi huo wa mabao 3-0 umeipa Yanga mwanzo mzuri wa Kombe la Mapinduzi na kuonyesha wazi kuwa Wananchi wamekuja Zanzibar wakiwa na dhamira ya kutwaa taji hilo.