MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, amesema kuwa kucheza mechi mbili pekee hakuwezi kuwa kipimo cha kutathmini ubora wa kocha mkuu wa timu hiyo, Steve Barker, huku akisisitiza kuwa uongozi hauko tayari kumuwekea presha mapema.
Mangungu amebainisha kuwa Barker ametambulishwa hivi karibuni kama kocha mkuu wa Simba, jukumu lake rasmi lilianza katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar, hivyo bado ni mapema kutoa tathmini ya kina kuhusu uwezo wake.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, suala la kuridhika au kutoridhika na kocha halipaswi kuamuliwa kwa kuangalia michezo miwili pekee, hali ya kikosi pia haijakaa sawa kutokana na wachezaji nane hadi tisa kukosekana.
“Hatuwezi kumpima kocha kwa mwenendo huo, hasa timu ikiwa imecheza mechi mbili tu na bado wachezaji wengi muhimu hawapo kikosini,” amesema Mangungu.
Ameongeza kuwa uongozi wa Simba umempa muda kocha Barker kuandaa kikosi chake kwa utulivu, kwa lengo la kujenga timu imara itakayokabiliana na mashindano makubwa yaliyo mbele, ikiwemo michuano ya kimataifa.
Akizungumzia mchezo wa jana dhidi ya Fufun SC, Mangungu amesema Simba ilimaliza salama licha ya changamoto chache za kiufundi zilizojitokeza, akiamini kuwa kocha Barker atazifanyia kazi kwa kina.
“Ni kweli timu ilicheza chini ya kiwango kwa baadhi ya nyakati, wachezaji walionekana kuwa na uoga kidogo wakifikiria mashindano ya kimataifa na hivyo kucheza kwa tahadhari ili kuepuka majeraha,” amesema Mwenyekiti huyo.