Home Habari za michezo UKUTA WA SINGIDA UNAVUJA, KOCHA ATIA NENO

UKUTA WA SINGIDA UNAVUJA, KOCHA ATIA NENO

33
0

SINGIDA Black Stars imeondoshwa hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, huku safu yao ya ulinzi ikionekana kutokuwa imara katika kujilinda.

Timu hiyo iliyokuwa kundi A na kumaliza nafasi ya pili, hadi inaondoshwa hatua ya nusu fainali kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, imeruhusu bao kila mechi.

Ikiwa imecheza mechi nne, imefunga mabao matano na kuruhusu manne ikiwa na wastani wa kila mechi nyavu zake kutikiswa.

Hali hiyo imemfanya kocha mkuu wa kikosi hicho, David Ouma kusema wanakwenda kulifanyia kazi, huku akifichua kwamba inachangiwa na maingizo mapya yanayohitaji muda kuelewana.

“Kikosi chetu kina maingizo mapya ambayo tumeanza kuyatumia katika mashindano haya, lakini wamefanya vizuri, tunaendelea kuboresha kila eneo, pia kumbuka kuna wachezaji hatupo nao kwa sababu mbalimbali ikiwamo kwenda kushiriki AFCON,” amesema Ouma.

Katika safu ya ulinzi ya Singida, mechi ya kwanza dhidi ya Mlandege, iliundwa na kipa Metacha Mnata, huku mabeki wakiwa Ande Koffi, Gadiel Michael, Kennedy Juma na Abdallah Kheri ‘Sebo’. Matokeo yalikuwa Singida 3-1 Mlandege.

Ilipocheza dhidi ya Azam na kutoka sare ya bao 1-1, ilikuwa hivi; Metacha, Koffi, Gadiel, Kennedy na Abdulmalick Zakaria.

Dhidi ya URA katika sare nyingine ya 1-1, safu hiyo ilikuwa na Metacha, Koffi, Gadiel, Sebo na Abdulmalick, kisha dhidi ya Yanga ilipofungwa 1-0 hatua ya nusu fainali, ilikuwa Metacha, Koffi, Ibrahim Imoro, Kennedy na Abdulmalick.

Katika safu hiyo ya ulinzi, Abdulmalick na Sebo ni maingizo mapya, huku Imoro akirejea kipindi hiki akitokea Mtibwa Sugar alipokuwa akicheza kwa mkopo.