MENEJA Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi cha timu hiyo kimerejea rasmi katika uwanja wa mazoezi kuanza maandalizi ya hatua zinazofuata za mashindano mbalimbali yanayowakabili.
Simba wanajiandaa na mchezo wa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaochezwa Januari 23, ugenini.
Ahmed amesema kurejea huko ni sehemu ya mpango wa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Steve Barker kuhakikisha wachezaji wanakuwa tayari kimwili na kiakili baada ya mapumziko mafupi yaliyotolewa ili kurejesha nguvu na kuondoa uchovu wa ratiba ngumu ya mechi.
“Mazoezi hayo yameanza kwa kasi nzuri, huku wachezaji wakionyesha ari kubwa na morali ya hali ya juu, jambo linalotoa picha chanya kwa benchi la ufundi kuelekea michezo ijayo ya ushindani,” amesema.
Ahmed amesema benchi la ufundi linaendelea kufanya tathmini ya kina kwa kila mchezaji ili kuhakikisha wote wako katika hali bora ya utimamu, huku programu maalum zikitumika kwa wachezaji waliokuwa wakisumbuliwa na majeraha madogo.
Ameongeza kuwa lengo kubwa la Simba ni kuendelea kupambana katika mashindano yote wanayoshiriki, maandalizi haya ni muhimu ili kuhakikisha timu inabaki katika kiwango cha juu na kutimiza malengo yake ya msimu.
Amewatoa hofu mashabiki wa Simba kwa kusema kuwa hali ya kikosi kwa ujumla ni nzuri, hakuna majeruhi wapya wakubwa waliopatikana wakati wa kurejea mazoezini.
Amewataka mashabiki kuendelea kutoa sapoti yao ya dhati kwa timu, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kuongeza hamasa kwa wachezaji wanapojiandaa kuwakilisha nembo ya Simba katika viwanja mbalimbali.