TAMATI ya Kombe la Mapinduzi 2026 ilikuwa jana Jumanne Januari 2026 ilipopigwa mechi ya fainali kati ya Azam dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kuanzia saa 10:30 jioni.
Kabla ya kupigwa mechi ya fainali ya michuano hiyo iliyoanza Desemba 28, 2025, kulikuwa na nyota wanne waliovuja jasho kwa kucheza mechi zote hadi kutinga hatua ya mwisho.
Wachezaji hao ni makipa Aboutwalib Mshery (Yanga) na Aishi Manula (Azam) pamoja na mabeki Chadrack Boka na Frank Assinki wote wanakipiga Yanga.
Mshery ambaye katika mechi tatu alizodaka zikiwamo mbili hatua ya makundi na moja nusu fainali, amefanikiwa kuondoka bila ya kuruhusu bao. Ndiye kipa mwenye clean sheet nyingi katika mashindano ya mwaka huu ambazo ni tatu alizopata dhidi ya KVZ, TRA United na Singida Black Stars.
Kwa upande wa Manula, ameidakia Azam mechi zote nne kwa dakika 360. Katika mechi hizo tatu ni hatua ya makundi na moja nusu fainali, akiruhusu mabao mawili dhidi ya Singida Black Stars na URA hatua ya makundi, huku akiwa na clean sheet mbili alizopata dhidi ya Mlandege (makundi) na Simba (nusu fainali).
Boka na Assinki, ndiyo mabeki ambao wamecheza mechi zote tatu za Yanga bila ya kufanyiwa mabadiliko wakiungana na Mshery kuwa nyota pekee wa kikosi hicho kucheza dakika zote 270.
Wakati huohuo, nyota wawili, Tusuubira Abraham wa URA na Adam Omar Adam wa TRA United wakiweka rekodi ya wachezaji walioingia kutokea benchi, lakini hawakumaliza mechi, wakatolewa baada ya muda kidogo kukichafua.Alianza Adam wakati TRA United ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KVZ mechi ikichezwa Desemba 29, 2025, dakika ya 57 aliingia kuchukua nafasi ya James Msuva, akatolewa dakika ya 80 kumpisha Shaban Chilunda. Dakika 23 pekee zilimtosha kuonekana.Tusuubira naye alikutana na hali kama hiyo wakati URA ikifungwa 2-1 na Azam, Januari 5, 2026 ambapo dakika ya 60 aliingia kuchukua nafasi ya Aliro Moses, akatolewa dakika ya 89 kumpisha Amaku Fred. Alicheza kwa dakika 29 pekee.