Home Habari za michezo SIMBA IKO NJIANI KUREJESHA HESHIMA, AHMEDY

SIMBA IKO NJIANI KUREJESHA HESHIMA, AHMEDY

21
0

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema ana imani kubwa kuwa timu yao itafanya vizuri na hatimaye kurejesha heshima yake kwa kutwaa taji kubwa hapa nchini, licha ya kipindi kigumu walichopitia katika misimu ya hivi karibuni.

Amesema kwa msimu wa tano mfululizo Simba haijafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sambamba na kushindwa kutwaa Kombe la Mapinduzi, lakini akasisitiza kuwa kila jambo lina wakati wake na mafanikio hayaji kwa pupa.

Ahmed amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa wavumilivu, akieleza kuwa ana uhakika Simba itarejea kwenye mstari wa ushindi na kunyakua kombe kubwa, licha ya kupoteza uhalisia wa kutwaa mataji kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza kuhusu ushiriki wa Simba katika Kombe la Mapinduzi, Ahmed alisema walikuwa na malengo mawili makubwa, ikiwemo kumpa nafasi kocha mkuu Steve Barker kuwajua wachezaji wake na mfumo wa timu.

Alifafanua kuwa Barker ni kocha mpya aliyeanza kazi rasmi Desemba 28, na kufikia Januari 3, 2026 Simba tayari ilikuwa ikicheza mechi za Kombe la Mapinduzi, hali iliyomnyima muda wa kutosha wa kukaa na kikosi na kukiweka sawa.

“Tungefurahi kutwaa Kombe la Mapinduzi kama ingetokea, lakini haikuwa bahati yetu. Hatuna sababu ya kujilaumu, badala yake tunaendelea kusonga mbele na mipango yetu ya baadaye, ikiwemo kuandaa timu kwa mashindano mengine,” amesema Ahmed.

Kwa sasa, kikosi cha Simba kimeingia kambini kikijiandaa na mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia, huku matarajio yakiwa ni kufanya vizuri na kuanza safari mpya ya mafanikio.