“Timu inaendelea vizuri na kwa mujibu wa ratiba tutakuwa na mechi mbili za ligi kabla ya michuano ya kimataifa, hivyo tutazitumia hizo kuhakikisha tunakuwa bora kabla ya kuivaa AS Otoho d’Oyo,” amesema Ouma na kuongeza;
“Ninachofurahia ni kwamba timu ipo kwenye hali nzuri ya utimamu baada ya kutoka kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kukosa baadhi ya wachezaji sasa timu imekamilika na inaendelea na maandalizi.”
Kocha huyo raia wa Kenya, aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyepandishwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo huku akiendelea kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars, amesema anatarajia kupata ushindani wa kutosha kutoka kwa Dodoma Jiji na JKT Tanzania timu hizo ndio zitakazotoa picha ya timu yake itaikabiri vipi AS Otoho ikiwa uwanja wa nyumbani.“Ligi yetu ni bora na yenye ushindani, ilianza vyema msimu huu nafikiri kutakuwa na muendelezo bora baada ya kurejea tena, sitarajii mechi rahisi hata wachezaji wanatambua hilo hivyo tunafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunakuwa bora na imara tayari kwa ushindani.”
Singida iliyotolewa nusu fainali ya Mapinduzi 2026 na Yanga iliyobeba ubingwa juzi usiku kwa kuifunga Azam FC kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu, kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ikiwa na pointi nane kupitia mechi tano.
Katika michuano ya Shirikisho Afrika inashika mkia katika Kundi C ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili ikiambulia sare moja na kupoteza mbele ya CR Belouizdad yenye alama tatu ikiwa ya tatu nyuma ya As Otoho na Stellenbosch zenye pointi nne kila moja kwa sasa.
Singida itacheza na As Otoho mechi mbili mfululizo, kwani baada ya kuwa wenyeji Januari 25 itasafiri kuifuata jijini Brazzaville kuruidiana kabla ya kujiandaa kumalizia mechi mbili za mwisho za kundi dhidi ya Stellenbosch na Belouizdad ili kusaka tiketi ya robo fainali.