Home Habari za michezo AHMEDY AFICHUA SIRI YA BEKI MPYA MSIMBAZI

AHMEDY AFICHUA SIRI YA BEKI MPYA MSIMBAZI

1682
0

LICHA ya uongozi wa Simba SC kuendelea kulihifadhi jina la beki mpya waliyekamilisha naye makubaliano, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa Wekundu wa Msimbazi wamepata mchezaji sahihi kwa ajili ya kuimarisha safu ya ulinzi.

Ahmed amesema usajili uliofanywa katika dirisha dogo ni wa kimkakati na unaenda kuipa Simba nguvu mpya, hususan katika maeneo ya ulinzi ambayo yalikuwa yakihitaji maboresho kuelekea mashindano yajayo ya ndani na kimataifa.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa Simba wamekamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa kati wa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, Ismael Oliver Touré, ambaye kwa sasa alikuwa akiitumikia klabu ya Baniyas inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za Kiarabu (UAE).

Ingawa Ahmed hakutaja jina la beki huyo hadharani, ameeleza kwa msisitizo kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anayefaa kabisa katika falsafa ya Simba, akimtaja kwa sifa ya kipekee inayodhihirisha uimara wake uwanjani.

“Usajili ambao tumefanya Simba katika dirisha dogo ni hatari. Kuna mtu mwili nyumba, huyo anacheza nafasi ya beki, anacheza kulia na kushoto pia,” alisema Ahmed, akionyesha imani kubwa na chaguo la klabu.

Kauli hiyo imezidi kuwapa matumaini mashabiki wa Simba kuwa uongozi wao umefanya kazi kubwa sokoni na kwamba beki huyo mpya atakuwa mhimili muhimu katika kikosi kitakachopambana kutetea heshima ya klabu kwenye mashindano mbalimbali.