UONGOZI wa klabu ya Yanga SC umemtambulisha rasmi aliyekuwa kipa wa Singida Black Stars na timu ya Taifa Stars, Hussein Masalanga, kama mchezaji mpya wa kikosi hicho kuelekea msimu unaoendelea na michuano ijayo ya ndani na kimataifa.
Masalanga ametua Yanga baada ya kuonyesha kiwango bora akiwa na Singida Black Stars, ambapo alijijengea jina kwa utulivu, ujasiri na uwezo wa kuongoza safu ya ulinzi akiwa langoni.
Uongozi wa Yanga umeeleza kuwa usajili wake ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi na kuongeza ushindani katika nafasi ya ulinzi wa lango.
Mbali na mafanikio yake ya klabu, Masalanga pia amewahi kuitumikia timu ya Taifa Stars, ambapo alipata nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika mashindano ya AFCON.
Katika michuano hiyo, alionesha kiwango cha juu kwa kuokoa mipira migumu na kusaidia timu kupata matokeo chanya, jambo lililovutia macho ya wadau wengi wa soka.
Masalanga ana uzoefu, uwezo wa kiufundi na kisaikolojia unaohitajika katika mechi kubwa. uwepo wake utaongeza ushindani mzuri miongoni mwa makipa na kuinua kiwango cha jumla cha kikosi.
Kwa ujio wa Masalanga, Yanga inaendelea kuonesha dhamira yake ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa.
Mashabiki wa klabu hiyo wanatarajia kumuona kipa huyo akitoa mchango mkubwa mara atakapopewa nafasi ya kulinda lango la Wananchi.