City haijaanza vizuri sana msimu huu kulinganisha na mpinzani wake kwani inakamata nafasi ya 13 ikikusanya pointi nane zilizotokana na kushinda mechi mbili na sare mbili, ikipoteza nane. Imefunga mabao saba na kuruhusu 13 ikishuka dimbani mara kumi.
Rekodi zinaonyesha kuwa, msimu wa mwisho 2022-2023 timu hizo kukutana Ligi Kuu Bara kabla ya kila moja kushuka kwa wakati wake, City ilifanya vizuri dhidi ya Mtibwa ikikusanya pointi nne baada ya kutoka 2-2, kisha ikashinda bao 1-0.
Tangu msimu wa 2013-2014, timu hizo zimekutana mara 20, Mtibwa Sugar ikishinda sita, City nayo imeibuka na ushindi mara tano, huku sare zikiwa tisa.
Jumla ya mechi 23 zimechezwa baina ya timu hizo katika Ligi Kuu (20), Championship (2) na Kombe la FA (1), huku ikishuhudiwa mara tano pekee zikitoka uwanjani bila ya nyavu kutikiswa, hivyo zinapokutana, ishu ya kufunga bao ipo kwa asilimia kubwa.
Kocha Mecky Maxime, huu ni mtihani wake wa kwanza tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo Desemba 7, 2025 akichukua nafasi ya Malale Hamsini.
Maxime ana mtihani wa kuhakikisha City inapata matokeo mazuri kwani mechi yano za mwisho, imekusanya pointi moja, ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Tanzania, baada ya hapo ikafungwa na Mashujaa (1-0), ikachapwa 2-0 na Coastal Union, kisha ikapokea kipigo cha 1-0 kutoka Namungo, ikahitimisha na kufungwa 3-0 dhidi ya Simba.
Mtibwa mechi tano za mwisho imekusanya pointi sita ikipoteza mechi moja pekee dhidi ya Yanga ilipofungwa 2-0. Baada ya hapo, matokeo yalikuwa hivi; KMC 0-0 Mtibwa, Mtibwa 2-1 TRA, JKT 0-0 Mtibwa na Simba 1-1 Mtibwa.