MUDA mchache baada ya Singida Black Stars kukubali kumwachia Clatous Chama atimkie Simba, uongozi wa klabu hiyo upo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kiungo Mkongomani, Linda Mtange kutoka Aigles Du Congo.
Chama aliitumikia Singida Black Stars kwa miezi sita akitua mwanzoni mwa msimu huu akitokea Yanga na alihudumu kwa msimu mmoja akitokea Simba.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida Black Stars, kililiambia Mwanaspoti, wamemwachia Chama baada ya kupata mbadala sahihi ambaye ataweza kuipa vitu vingi zaidi ndani ya timu yao.“Ni kweli Chama anaondoka Singida Black Stars dirisha hili na tayari tumeshampata mbadala wake ambaye tunaamini ataweza kufanya mambo makubwa ndani ya timu, makubaliano ya kumalizana na kiungo huyo yapo katika hatua za mwisho.
“Kuhusu Chama tumemalizana vizuri na makubaliano ya pande zote mbili pia yamekwenda vizuri, kilichobaki sasa ni kila pande kukamilisha mchakato tuliokubaliana,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema mabadiliko yanayofanywa yanazingatiwa na benchi la ufundi ambalo tayari limeona ubora wa nyota waliotoka akimtaja Nickson Kibabage na Chama na kuamua kufanya uamuzi wa haraka kusajili warithi wao.
“Kibabage kaondoka tayari tulikuwa tumeongeza nguvu eneo lake kwa kumnasa beki kutoka KMC, Abdallah Said ‘Lanso’ na sasa Chama katoka chaguo ni Mtange,” kimebainisha chanzo hicho.