Home Habari za michezo MNYAMA CHAMA AREJEA UNYAMANI

MNYAMA CHAMA AREJEA UNYAMANI

140
0

BAADA ya Klabu ya Simba SC kumtambulisha rasmi kurejea kwa kiungo mshambuliaji Clatous Chama, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kurejea kwa nyota huyo ni ishara kuwa kiongozi halisi wa kikosi amerejea nyumbani.

Chama amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga tena na Wekundu wa Msimbazi akitokea Singida Black Stars, ambapo alikuwa akitumikia klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake wa awali wa mwaka mmoja. Awali, mchezaji huyo aliwahi pia kupitia Yanga kabla ya kurejea tena ndani ya Simba.

Ahmed alisema kurejea kwa Chama kunakwenda kurejesha heshima na ubora wa Simba, amesisitiza kuwa hakuna sehemu nyingine ambayo mchezaji huyo anaweza kuonyesha uwezo wake mkubwa kama ilivyo ndani ya klabu hiyo.

“Mwenda tezi na omo, marejeo ngamani. Kila kitu kizuri kimerejea ndani ya Simba. Karibu sana Mwamba, tulikuhitaji sana katika nyakati hizi,” alisema Ahmed huku akionyesha imani kubwa na mchango wa nyota huyo.

Ameongeza  kuwa furaha imerejea Msimbazi, Chama ni mchezaji mwenye ubora wa hali ya juu ambaye alipoondoka hakuweza kuonyesha kiwango chake cha kweli, lakini sasa amerudi nyumbani tayari kuendeleza yale ambayo mashabiki wa Simba wamezoea.

“Chama ni mkongwe ndani ya kikosi cha Simba, ni mchezaji aliyewahi kutupeleka robo fainali kwa mara ya kwanza. Amerudi kuwaambia wenzake kuwa sasa ni wakati wa kuipigania Simba kwa nguvu zote,” amesema.

Kwa mujibu wa Ahmed, kurejea kwa Chama ni hatua muhimu katika dhamira ya kurejesha heshima ya Simba,  kuwa kiongozi huyo amerejea kuongoza wenzake na kupambana kwa ajili ya bendera ya Msimbazi katika mashindano yote yanayokuja.