Home Habari za michezo HALI YA HEWA SIO KIKWAZO KWA WACHEZAJI, ETUTU

HALI YA HEWA SIO KIKWAZO KWA WACHEZAJI, ETUTU

42
0

DAKTARI wa klabu ya Yanga, Moses Etutu, ameweka wazi kuwa benchi la afya la timu hiyo linaendelea kufanya kazi kubwa kuhakikisha wachezaji wanazoea na kudhibiti hali ya hewa ya nchini Misri.

Yanga kwa sasa ipo nchini humo ikiwa katika maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Al Ahly, unaotarajiwa kuchezwa kesho katika uwanja wa Cairo.

Etutu amesema moja ya changamoto kubwa wanayokutana nayo ni hali ya hewa ya baridi iliyopo Misri, tofauti na hali ya hewa ambayo wachezaji wengi wameizoea nchini Tanzania.

Amefafanua kuwa timu ya madaktari na benchi la ufundi wamechukua tahadhari zote muhimu kuhakikisha wachezaji wanajenga mwili na kuzoea mazingira mapya ili kuepuka athari zozote zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Kufika mapema kumesaidia sana, kwa sababu kumewapa wachezaji muda wa kuzoea hali ya hewa ya huku na hivyo kupunguza uwezekano wa kuathiriwa na baridi siku ya mechi,” amesema Etutu.

Kwa mujibu wa daktari huyo, maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha Yanga inaingia uwanjani ikiwa katika hali bora ya kimwili na kiafya, tayari kupambana na Al Ahly katika mchezo unaobeba uzito mkubwa kwenye michuano hiyo ya kimataifa.