Home Habari za michezo SIMBA YAMALIZANA NA MASHINE MBILI

SIMBA YAMALIZANA NA MASHINE MBILI

36
0

UONGOZI wa Klabu ya Simba unaelezwa kuwa upo hatua za mwisho kukamilisha usajili wa wachezaji wawili wapya, kiungo mshambuliaji IƱno Jospin Loemba pamoja na winga Alain Anicet Oura, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya kikosi kuelekea michezo ijayo ya ndani na kimataifa.

Loemba ni raia wa Congo Brazzaville anayekipiga katika klabu ya Colombe Sportive du Dja et Lobo ya nchini Cameroon, inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Rekodi zinaonyesha mchezaji huyo amewahi kucheza mechi nne za michuano ya CAF na kufanikiwa kufunga bao moja, akionesha uwezo wa kuchangia katika safu ya ushambuliaji.

Kwa upande wa Oura, ametokea katika klabu ya IF Gnistan ya Daraja la Kwanza nchini Finland. Mchezaji huyo ana uwezo wa kucheza nafasi ya winga wa kulia na kushoto, akitambulika kwa kasi, chenga pamoja na uwezo wa kutengeneza nafasi za mabao.

Inaelezwa kuwa Oura anaifahamu vyema falsafa ya Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, kutokana na kufanya naye kazi awali wakiwa katika klabu ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, jambo linalotarajiwa kumpa urahisi wa kuingia haraka kwenye mfumo wa timu.

Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa Simba tayari imekamilisha taratibu muhimu za usajili wa wachezaji hao wawili, huku pia ikiwa na mpango wa kufanya mabadiliko makubwa kwa kuwaacha baadhi ya mastaa ili kupisha sura mpya ndani ya kikosi.

Chanzo cha kuaminika kimeeleza kuwa uongozi wa klabu unaamini nyota hao wapya wataongeza ushindani na nguvu mpya, hasa baada ya kuondoka kwa baadhi ya wachezaji akiwemo Steven Mukwala na Joshua Mutale.

Hadi sasa kupitia dirisha dogo la usajili, Simba tayari imetambulisha wachezaji watano wapya ambao ni Libasse Gueye, Ismael Olivier Toure, Djibrila Kassali, Clatous Chama na Nickson Kibabage, huku mashabiki wakingoja kwa hamu kutangazwa kwa nyongeza zaidi.