MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho bado kina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya changamoto zilizojitokeza kwenye michezo ya awali.
Ahmed ameeleza kuwa Simba imebakiwa na fursa moja muhimu ya dhahabu, hususan katika mchezo wa marudiano wa nyumbani utakaochezwa Februari 01, akisisitiza kuwa matokeo ya mechi hiyo yatakuwa na mchango mkubwa katika mwelekeo wa timu hiyo kwenye kundi.
Simba inatarajia kushuka dimbani Februari Mosi mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikisaka ushindi dhidi ya Esperance Sportive de Tunis katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki.
Mbali na mchezo huo wa nyumbani, Simba pia itakuwa na kibarua kingine kigumu cha kusaka alama sita dhidi ya Petro de Luanda ugenini kabla ya kurejea nyumbani kuikabili Stade Malien, michezo ambayo imeelezwa kuwa ya msingi katika kufufua matumaini ya timu hiyo.
Ahmed amesisitiza kuwa michezo hiyo mitatu iliyobaki ni muhimu sana katika safari ya Simba ya kupigania kufuzu kwenda hatua ya robo fainali, akibainisha kuwa bado hakuna sababu ya kukata tamaa kwa kuwa kila kitu kiko wazi.
Ameongeza kuwa namna ambavyo Simba imekuwa ikicheza pamoja na juhudi kubwa zilizooneshwa na wachezaji katika michezo iliyopita, kunatoa matumaini makubwa ya kupata matokeo chanya kwenye michezo ya mwisho ya kundi.
Kwa mujibu wa Ally, klabu hiyo bado ina alama tisa za kupigania, na ni haki halali ya Simba kupambana kuhakikisha inazivuna zote. “Hatukati tamaa hata kidogo. Mechi tatu za mwisho ni halali yetu, bado tuna alama tisa za kupigania na sasa tunaianza safari mpya ya kuzifukuzia,” amesema
Amesema.kikosi cha Simba kimejipanga upya kisaikolojia na kimkakati, akionesha imani kubwa kuwa kwa msaada wa mashabiki na juhudi za wachezaji, timu hiyo itaweza kupata matokeo mazuri katika michezo iliyobaki.