KIKOSI cha klabu ya Simba kinarejea jijini Dar es Salaam kikitokea Tunis, Tunisia, ambako jana kilicheza mchezo wa mzunguko wa tatu wa Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis (ES Tunis).
Katika mchezo huo uliochezwa ugenini, Simba ilipoteza kwa bao 1-0, matokeo yaliyowaumiza mashabiki wa klabu hiyo waliokuwa na matumaini ya kuona timu yao ikipata angalau sare ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kupambana kwenye kundi hilo.
Kipigo hicho kimeifanya Simba kuendelea kuburuza mkia wa Kundi D bila pointi yoyote baada ya kucheza michezo mitatu, hali inayoongeza presha kwa kikosi na benchi la ufundi katika harakati za kusaka nafasi ya kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Hata hivyo, Simba bado ina nafasi ya kujirekebisha pale itakapopata fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya ES Tunis katika mchezo wa mzunguko wa nne wa Kundi D, utakaochezwa mwishoni mwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Kwa sasa, ES Tunis inaongoza Kundi D ikiwa na pointi tano, huku timu za Stade Malien na Petro Atlético, ambazo zinatarajiwa kukutana leo Jumapili Januari 25, kila moja ikiwa na pointi nne, hali inayoifanya Simba kulazimika kushinda michezo yake ya nyumbani ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele.