Home Habari za michezo SIMBA BADO HAIJAISHIWA PAWA CAF, AHMED ALLY

SIMBA BADO HAIJAISHIWA PAWA CAF, AHMED ALLY

42
0

MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutoishiwa matumaini licha ya matokeo ya kikosi hicho katika mashindano ya CAF msimu huu, amesisitiza kuwa bado kuna nafasi ya kufanya makubwa katika mechi zilizosalia za hatua ya makundi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ahmed Ally amesema ametua jijini Dar es Salaam akitokea Tunisia na mara baada ya kufika nchini alijikuta akijaa matumaini mapya baada ya kuona mapokezi na mapenzi ya mashabiki wa Simba katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Ameeleza kuwa mazingira ya jiji la Dar es Salaam pamoja na joto la mashabiki yameongeza ari na imani kwake kuwa timu hiyo bado ina uwezo wa kufanya vizuri katika mechi tatu za mwisho za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ahmed ameongeza kuwa kuanzia Jumapili, Februari 01, Simba itaanza safari mpya ya kuandika historia itakayotikisa na kushangaza Afrika, akisisitiza kuwa ndoto ya kufuzu robo fainali bado ipo hai na haiko katika ndoto bali katika mipango madhubuti ya klabu.

Amewataka Wanasimba kuendelea kuiunga mkono timu yao kikamilifu ili kufanikisha azma ya kufuzu robo fainali kwa mara ya nane mfululizo, akisisitiza kuwa mshikamano wa mashabiki ni silaha kubwa kwa kikosi hicho.

Ujumbe wake, Ahmed  amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuishiwa pawa, huku akiwataka mashabiki wote wa Simba kubeba matumaini hayo na kuingia kwenye mapambano kwa imani, akimalizia kwa kauli mbiu “HatujaishiwaPawa”.