Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi kuwa hana mashaka na usajili mpya uliofanywa na uongozi wa klabu hiyo katika kipindi cha dirisha dogo la usajili, akisisitiza kuwa wachezaji waliopatikana wana ubora unaohitajika kuisaidia timu katika mashindano mbalimbali.
Barker amesema usajili huo umezingatia mahitaji halisi ya kikosi, huku akieleza kuwa lengo kuu lilikuwa kuongeza ushindani wa ndani na kuimarisha maeneo yaliyohitaji maboresho zaidi ili Simba iwe imara kwa michezo inayokuja.
Katika dirisha hilo dogo, Simba imefanikiwa kuwasajili nyota kadhaa akiwemo Libasse Gueye, Ismael Olivier Toure, Djibrila Kassali, Clatous Chama pamoja na Nickson Kibabage, wachezaji ambao kocha huyo anaamini watatoa mchango mkubwa ndani ya timu.
Kocha Barker ameongeza kuwa ana imani kubwa na uwezo wa wachezaji hao wapya, akieleza kuwa wamekuja na morali nzuri pamoja na ari ya kupambana ili kuthibitisha thamani yao ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Amesema usajili huo tayari umeanza kuleta tija kwenye maandalizi ya timu, huku akibainisha kuwa kila mchezaji ameonyesha dalili chanya katika mazoezi na anaelewa falsafa ya mchezo anayoitaka Simba icheze.
“Usajili wote umenilipa na ni wakati sahihi sasa wa mimi kutumia wachezaji wangu vizuri kwa ajili ya michezo ya nyumbani,” amesema Barker, akisisitiza kuwa anaamini Simba itaonekana tofauti na yenye ushindani mkubwa katika michezo ijayo.