NYASI za Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge zinatarajiwa kuwaka moto leo, Yanga SC ikiwakaribisha Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Yanga, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, wanashuka dimbani wakiwa nyumbani wakilenga kuondoka na pointi tatu muhimu ili kuendelea kujihakikishia nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa msimu huu. Mchezo huu ni fursa kwao kuimarisha msimamo wao baada ya ratiba ngumu ya michezo ya kimataifa.
Kwa upande wa benchi la ufundi, Yanga inanolewa na Kocha Pedro Gonçalves, huku Dodoma Jiji FC ikiongozwa na kocha Mtanzania, Aman Josiah. Kila upande unaingia uwanjani ukiwa na kiu ya pointi, jambo linaloashiria pambano kali la dakika 90.
Kuelekea mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, amesema kikosi chake kimepata muda mfupi wa maandalizi kutokana na safari ndefu na mchezo wa ugenini dhidi ya Al Ahly, lakini wamejitahidi kurejea haraka kwenye mwelekeo wa ligi.
Mabedi ameongeza kuwa licha ya changamoto ya muda, Yanga inajivunia kuwa na kikosi kipana chenye wachezaji wenye uwezo wa kukabiliana na presha ya ratiba, hivyo wako tayari kwa mchezo wa leo.
“Tunajua umuhimu wa mchezo huu. Matokeo ya mchezo uliopita hayawezi kutuathiri kwenye mipango yetu. Kwa asilimia kubwa wachezaji wako sawa kiafya na wako tayari kupambana,” alisema Mabedi,