Home Habari za michezo YANGA TUPO TAYARI KWA VITA NA AL AHLY, PEDRO

YANGA TUPO TAYARI KWA VITA NA AL AHLY, PEDRO

3
0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kikosi chake kimefanya maandalizi ya kutosha uwanjani na kwa sasa kipo katika hatua ya mwisho ya maandalizi kuelekea mchezo muhimu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Yanga itashuka dimbani kesho katika mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo inahitaji matokeo chanya ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye kundi lake gumu la michuano hiyo.

Pedro amesema  kama mchezo ungechezwa leo, angeweza kusema kikosi chake kipo tayari kabisa, kwa kuwa  wachezaji wake wako tayari kucheza mpira mzuri kesho, lakini kwa heshima kubwa kwa wapinzani wao ambao pia ni timu yenye ubora na uzoefu mkubwa barani Afrika.

“Kabla ya yote, tulipopangwa kwenye kundi hili kila timu ilijua ipo kwenye kundi gumu. Sisi kama Yanga kazi yetu ni kupambana na kila timu ili kujiweka kwenye nafasi nzuri. Tunapaswa kuwa bora, makini na tayari kucheza mpira mzuri,” amesema Pedro.

Akizungumzia mchezo wa kwanza, kocha huyo amesema Yanga ilicheza vizuri lakini ilifanya makosa machache ambayo Al Ahly walitumia vyema kutokana na ubora wao.

Amesisitiza kuwa kwenye mchezo wa kesho, Yanga inapaswa kuonesha ukuaji, umakini na kiwango bora zaidi ili kupata ushindi.

Pedro ameongeza kuwa wanatambua watakuwa wanakutana na timu kubwa,  wanajua kutakuwa na nyakati tofauti ndani ya mchezo, zikiwemo nyakati ambazo watakuwa na umiliki wa mpira na nyakati ambazo Al Ahly watatawala mchezo.

Amesema umuhimu wa kuwa makini katika kila hatua, iwe ni wakati wa kushambulia au kujilinda, ili kufanikisha lengo lao la kushinda mchezo huo muhimu.