BAADA ya uongozi wa Klabu ya Yanga kufunga dirisha la usajili kwa kumtambulisha winga wa kulia, Buba Jammeh, mabingwa hao wa Tanzania wameendelea kuonyesha dhamira yao ya dhati ya kuimarisha kikosi.
Buba amejiunga na Yanga akitokea Interclube ya Angola, usajili unaoonekana kuongeza nguvu na ushindani ndani ya timu. Yanga inaendelea kuthibitisha kuwa ni moja ya timu zilizo kwenye ubora wa hali ya juu, hali inayowafanya wapinzani wao kukosa usingizi.
Kila idara ya kikosi imeonekana kuwa imara, huku benchi la ufundi likionyesha mipango madhubuti ya kuhakikisha timu inakuwa na ushindani mkubwa katika mashindano yote wanayoshiriki.
Usajili wa Buba Jammeh ni sehemu ya mkakati wa Yanga wa kuendelea kuimarisha kikosi chao ili kuwa tishio kubwa kwa wapinzani, siyo tu katika ligi za ndani bali pia kwenye michuano ya kimataifa. Kasi, uwezo wa kupambana na ujasiri wake uwanjani vinatarajiwa kuongeza chaguo zaidi kwa benchi la ufundi.
Ujio wa winga huyo wa kulia unaifanya safu ya ushambuliaji kuwa imara zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa upande wa kushoto tayari upo mikononi mwa Max Nzengeli, ambaye amekuwa akionyesha kiwango cha juu na mchango mkubwa kwa timu.
Mchanganyiko wa Buba kulia na Nzengeli kushoto na wengine unaipa Yanga nguvu mpya na upana mkubwa katika kufanya mashambulizi.
Kila Yanga wanaposhuka dimbani, wamekuwa wakionyesha soka la kasi, nidhamu na mipango iliyo wazi ya kushinda. Mabadiliko chanya ndani ya kikosi tayari yameanza kuzaa matunda mapema, ishara tosha kuwa timu hiyo ina kiu kubwa ya mafanikio makubwa msimu huu.