HATMA ya kiungo wa Simba SC, Mpanzu, bado ipo gizani baada ya mazungumzo ya uhamisho wake na klabu ya CR Belouizdad ya Algeria kufeli kufikia makubaliano.
Hali ambayo iliyoongeza sintofahamu juu ya mustakabali wa mchezaji huyo ndani ya dirisha dogo la usajili ambalo limefungwa juzi.
Taarifa zinaeleza kuwa pamoja na CR Belouizdad kuonyesha nia ya dhati ya kumnasa Mpanzu, pande hizo mbili zimeshindwa kukubaliana vigezo muhimu vya dili hilo, jambo lililosababisha mazungumzo kusimama bila mafanikio hadi sasa.
Wakati huo huo, Simba imeendelea kuonyesha msimamo mkali sokoni baada ya kuikatalia Raja Casablanca ya Morocco, pia iliwasilisha ofa ya kumchukua mchezaji huyo, lakini uongozi wa wekundu wa Msimbazi ukaona haikuwa na maslahi kwa klabu.
Kutokana na hali hiyo, Mpanzu anaendelea kubaki ndani ya kikosi cha Simba, huku benchi la ufundi likimtazama kama sehemu muhimu ya mipango ya timu katika mashindano yanayoendelea, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mashabiki wa Simba sasa wanasubiri kwa hamu kuona iwapo klabu itabadilisha msimamo wake au kama Mpanzu ataendelea kuwa sehemu ya nguvu ya kikosi hicho, wakati dirisha la usajili likizidi kuingia katika hatua za mwisho.