Home Habari za michezo YANGA YAJIPANGA MOROCCO, LEO ROBO FAINALI

YANGA YAJIPANGA MOROCCO, LEO ROBO FAINALI

26
0

MENEJA wa Yanga, Walter Harrison, amesema kikosi cha timu hiyo kitaanza maandalizi mapema kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat, kwa kufanya mazoezi kesho Jumatatu kabla ya kusafiri Jumanne kwenda nchini Morocco.

Yanga wakitarajiwa kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya FAR Rabat Februari 7 nchini Morocco.

Harrison amesema safari hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Yanga inafanya vizuri katika mchezo huo mgumu wa ugenini, akisisitiza kuwa malengo ya klabu yako wazi kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Ameeleza kuwa hadi sasa Yanga imeshacheza michezo minne ya hatua ya makundi na kukusanya alama tano, ikishika nafasi ya tatu kwenye kundi. Kwa hali hiyo, amesema kilichobaki ni kuhakikisha wanatimiza malengo yao katika michezo miwili iliyosalia.

“Kwa sasa nguvu na akili zetu zote zimehamia kwenye michezo hiyo miwili. Ni lazima tuhakikishe tunacheza kwa kiwango cha juu kama tunataka kufikia robo fainali,” amesema Harrison

Meneja huyo ameongeza kuwa ana imani kubwa na kikosi walichonacho, akieleza kuwa ubora wa wachezaji pamoja na maandalizi mazuri yaliyofanywa na uongozi wa klabu vinatoa matumaini makubwa ya kufanikisha lengo hilo.

“Hakuna muda wa kupumzika, bado tuna safari ndefu kuelekea kufikia malengo yetu. Kila mtu ndani ya klabu anatambua ukubwa wa jukumu lililopo mbele yetu,” amesema Harrison.