Home Habari za michezo BOKA AOKOLEWA, NI MAKOSA YA TIMU NZIMA

BOKA AOKOLEWA, NI MAKOSA YA TIMU NZIMA

0

MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Alex Ngai, amemkingia kifua beki wa timu hiyo, Chadrack Boka, amesisitiza  kuwa makosa yaliyosababisha bao dhidi ya Al Ahly hayapaswi kumbebeshwa mchezaji mmoja bali ni ya timu nzima.

Ngai ametoa kauli hiyo kufuatia lawama zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya mashabiki wakidai kuwa Boka alihusika moja kwa moja katika kosa lililosababisha Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly, katika mchezo wa marudiano uliochezwa visiwani Zanzibar.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Ngai amesema bao hilo lilitokana na mpira wa kona uliodondoka katika eneo la hatari, jambo ambalo linahusisha safu nzima ya ulinzi na si beki mmoja pekee, kuwa makosa kama hayo ni sehemu ya mchezo wa mpira wa miguu.

“Kosa limefanyika kwa timu nzima, sio kosa la Boka peke yake. Ilikuwa ni kona, mpira ukadondoka kwenye eneo hatarishi na bao likafungwa,” amesema Ngai.

Ameongeza kuwa pamoja na matokeo hayo, Yanga ilionyesha kiwango kizuri dhidi ya wapinzani wao, kuwa Al Ahly ni timu yenye wachezaji wa kiwango cha juu licha ya wao pia kuwa na kikosi chenye ubora mkubwa.

“Al Ahly ni timu kubwa yenye wachezaji bora, lakini hata sisi tuna wachezaji wenye uwezo mkubwa. Ukiangalia baadhi yao mmoja mmoja, ni wachezaji wa daraja la juu kama Mohammed Trezeguet ambaye tayari ameshacheza katika ligi kubwa,” amesema.

Ngai amesema benchi la ufundi lilikuwa na mipango madhubuti kuelekea mchezo huo na matarajio yalikuwa ni kupata alama tatu, lakini hatimaye wakalazimika kuridhika na sare kutokana na makosa ambayo ni ya kawaida katika mchezo wa soka.

“Yote kwa yote, tulionyesha uwezo mkubwa na ushindani mkubwa. Tulikuwa na matumaini ya kushinda, lakini makosa hutokea na hayo ni sehemu ya mchezo,” amesema mjumbe huyo wa Kamati ya Utendaji ya Yanga.