Mayanga alijiunga na Mashujaa FC Machi 21, 2025, akitokea Mbeya City, akienda kuchukua nafasi ya kocha, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, ikiwa ni muda mfupi baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 3-0 na Singida Black Stars, Februari 26, 2025.
Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, msimu huu ameiongoza Mashujaa katika mechi 12 za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo ameshinda tatu, sare nne na kupoteza tano, ikifunga mabao matano na kuruhusu 13, ikiwa nafasi ya 10 kwa pointi 13.
Soka la Bongo lilimtafuta Ofisa Habari wa Mashujaa, Steven Ndorobo ambaye amesema bado wana nafasi ya kurekebisha makosa yao katika michezo ijayo, huu sio wakati wa kuikatia timu tamaa.
“Ni kweli tumepoteza mchezo wa tatu mfululuzo, lakini tunayo michezo mingine 18 mbele yetu ya kujisahihisha, huu sio wakati wa kulaumiana. Viongozi wanaona pia kinachoendelea na wanajua, na tunaumizwa pia na matokeo haya lakini ndio mpira.
“Tunautazama mchezo unaofuata dhidi ya Tanzania Prisons tunaokwenda kucheza Mbeya, timu imeshaanza safari ya kuwafuata wapinzani na tupo sambamba na kocha, yanayoendelea ni porojo tu,” amesema Ndorobo.