Home Habari za michezo MSIBA MOROCCO BUBA AMUACHA PEDRO NJIA PANDA

MSIBA MOROCCO BUBA AMUACHA PEDRO NJIA PANDA

0

NYOTA mpya wa Yanga, Buba Jammeh, anatarajiwa kutua nchini Tanzania kusubiri kikosi cha timu hiyo kitakaporejea kikitokea Morocco, ambako kipo kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat.

Awali, Buba alitarajiwa kuwasili jana Alhamisi katika jiji la Rabat ili kujiunga na kikosi cha Yanga kilichopo Morocco kwa maandalizi ya mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa kesho nchini humo, lakini mipango hiyo imeyeyuka.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, changamoto za kusafiri ndizo zilizokwamisha ujio wa nyota huyo, hali iliyosababisha ashindwe kuwapo kwenye mchezo dhidi ya AS FAR Rabat kama ilivyopangwa awali.

Kamwe amesema Buba alipaswa kuwasili Alhamisi na kuanza mazoezi na wenzake Ijumaa, jambo ambalo lingempa nafasi ya kuingizwa kwenye mipango ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Pedro Goncalves.

“Wakati tunamsajili Buba, alikuwapo Angola na alikamilisha mchakato wote ikiwemo vibali vya kusafiri, lakini alikumbana na changamoto zilizomlazimu kwenda Gambia kushughulikia hati yake ya kusafiria,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa benchi la ufundi lilikuwa na mpango wa kumpa nyota huyo nafasi ya kucheza kwenye mchezo wa Jumamosi, lakini kuchelewa kwake kumeharibu mpango huo.

“Hata hivyo, tumefuatilia safari yake na tumebaini atawasili Jumamosi, hivyo tumemuelekeza aunganishe safari moja kwa moja hadi Dar es Salaam ambako ataungana na timu,” ameongeza Kamwe.