Home Habari za michezo MWALIMU AJIPANGIA MABAO 15, ONYO KALI MABEKI LIGI KUU

MWALIMU AJIPANGIA MABAO 15, ONYO KALI MABEKI LIGI KUU

0

MSHAMBULIAJI wa Simba, Seleman Mwalimu, ameweka wazi malengo yake binafsi kwa msimu wa 2025/26, akijipangia kufunga zaidi ya mabao 15 mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania .

Nyota huyo anaamini ana uwezo wa kufikia idadi hiyo endapo ataendelea kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Hadi sasa, Mwalimu ameshatikisa nyavu mara tatu katika michezo nane ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo Simba imecheza, takwimu zinazoonyesha bado ana nafasi kubwa ya kuongeza idadi ya mabao kadri msimu unavyoendelea.

Akizungumza kuhusu malengo yake, Mwalimu amesema kila anapopata nafasi uwanjani, lengo lake ni moja tu, kufunga bao au kutengeneza pasi ya bao. mchango wake unapaswa kuonekana moja kwa moja kwenye matokeo ya timu.

“Kikubwa ni kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza. Kila ninapopata nafasi, nimejiwekea malengo ya kufunga au kutoa pasi ya bao. Hilo ndilo jambo la msingi kwangu,” amesema mshambuliaji huyo .

Ameongeza kuwa hawezi kuweka idadi maalum ya mabao kwa kila mechi, lakini ana uhakika siku akipata nafasi na mambo yakimwendea vizuri, anaweza hata kufunga hat-trick katika mchezo mmoja.

Mwalimu amesisitiza kuwa pamoja na Simba kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, morali ya kikosi ipo juu katika Ligi Kuu na mashindano mengine yaliyo mbele yao.

Amesema  wanaendelea kupambana kwa nguvu zote kuipigania nembo ya klabu hiyo hadi mwisho wa msimu kufikia malengo yanayotarajiwa.