KOCHA wa Yanga, Pedro Goncalves, hataki kupoteza muda kuelekea mchezo muhimu wa Jumapili dhidi ya JS Kabylie, baada ya kuanza kumpa majukumu maalum nyota wake mpya, Buba Jammeh, kwa ajili ya pambano hilo la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo utakaopigwa Dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, ili kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Hivyo, maandalizi yamekuwa makali huku benchi la ufundi likihakikisha kila mchezaji anakuwa tayari kwa vita hiyo.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, Buba ni miongoni mwa wachezaji watakaobeba jukumu la kuipambania nembo ya Yanga kuhakikisha timu inasonga mbele.
Amesisitiza kuwa ujio wa kiungo huyo unaongeza nguvu na chachu mpya ndani ya kikosi.
Kamwe amesema kikosi hicho kimeondoka tayari kuelekea Zanzibar kwa maandalizi ya mwisho, huku akieleza kuwa kocha Pedro amefanya kazi kubwa kuandaa kikosi imara kitakachokuwa na uwezo wa kuivusha Yanga katika hatua hiyo nyeti.
“Buba yupo ndani ya kikosi na tayari ameanza kupewa majukumu ya kuhakikisha Yanga inafuzu robo fainali kwa kuifunga JS Kabylie katika Dimba la New Amaan Complex siku ya Jumapili,” amesema Kamwe.
Hata hivyo, Yanga itamkosa Mohammed Damaro katika mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi aliyoipata katika mchezo uliopita, wakati wachezaji wengine wote wakiwa fiti na tayari kwa pambano hilo.