MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien utachezwa saa 1:00 usiku, tofauti na ilivyozoeleka kwa mechi nyingi kuanza saa 10:00 jioni.
Ahmed amesema mabadiliko hayo ya muda yametokana na kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambazo zinazitaka mechi zote za mwisho za hatua ya makundi kuchezwa kwa wakati mmoja ndani ya kundi husika ili kulinda ushindani wa haki na uwazi kwa timu zote.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Ahmed amesema kikosi tayari kimeanza maandalizi rasmi mara tu baada ya kumaliza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya KMC.
Wachezaji walirejea kambini na kuanza mazoezi, ambapo leo watafanya mazoezi katika Uwanja wa Mo Simba Arena kabla ya kuhitimisha kwa mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho yake.
Pamoja na kwamba Simba haina nafasi ya kusonga mbele katika michuano hiyo, Ahmed amesisitiza kuwa wameupa mchezo huo uzito mkubwa.
Amesema lengo lao ni kulinda heshima ya klabu na kuhakikisha wanaondoka katika hatua ya makundi wakiwa wameacha alama chanya. “Hatutaki kuona Simba inafanya vibaya zaidi. Tunataka kusimika heshima ya Mnyama,” amesema.
Ahmed amegusia rekodi ya Simba katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye michuano ya Afrika msimu huu, akieleza kuwa hawajapata ushindi wowote, jambo lililowakatisha tamaa baadhi ya mashabiki.
Amesema mchezo huo ni fursa adhimu ya kufuta taswira hiyo na kurejesha imani kwa mashabiki pamoja na wachezaji, akisisitiza kuwa Simba haipo tayari kupoteza mara mbili dhidi ya mpinzani mmoja.
“Tumewahi kufungwa na timu kama Al Ahly, lakini walipokuja Mkapa tuliwarudishia. Hiyo ndiyo falsafa ya Simba,” amesisitiza Ahmed, akiahidi kuwa kikosi kitapambana kuhakikisha kinapata ushindi dhidi ya Stade Malien.
Kwa upande wa mashabiki, Ahmed amewataka Wanasimba kujitokeza kwa wingi uwanjani Februari 14 kuipa timu sapoti.
Amesema licha ya kushindwa kufuzu robo fainali msimu huu, bado timu inahitaji nguvu yao ili kurejesha morali kuelekea michezo ijayo ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Kuhusu viingilio, Ahmed amesema vitakuwa kama kawaida: mzunguko ni Sh 3,000, VIP C Sh 5,000, VIP B Sh 10,000, VIP A Sh 20,000 na Platinum Sh 100,000.
Wakati huohuo, Stade Malien wanatarajiwa kuwasili nchini Februari 13 alfajiri na kufanya mazoezi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku hiyo kabla ya kushuka dimbani Februari 14 kumaliza rasmi hatua ya makundi. Waamuzi wa mchezo huo watatoka Malawi.
Ahmed amesem safari hii hamasa kubwa ipo kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuishangilia timu yao ili kumaliza hatua ya makundi kwa heshima na ari mpya.