MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Jonathan Sowah, ameondolewa kwenye kikosi kilichopo kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC, kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu ya kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa sakata hilo lilianzia kwenye utaratibu wa kawaida wa kocha wa viungo wa Simba, huwaandalia programu maalum ya mazoezi wachezaji wasiopata nafasi ya kucheza au wanaocheza dakika chache mara baada ya kila mechi kumalizika.
Lengo la utaratibu huo unaofanywa na benchi la ufundi la Simba kuhakikisha kila mchezaji anabaki kwenye kiwango bora cha utimamu wa mwili.
Inaelezwa kuwa kabla ya mchezo huo, kocha wa viungo aliwapa taarifa wachezaji wote, akiwemo Sowah, kubeba vifaa vya mazoezi ili washiriki programu hiyo baada ya mechi.
Sowah hakubeba vifaa hivyo na alipoulizwa sababu, alieleza kuwa angefanya mazoezi binafsi kwenye gym usiku.
Hatua hiyo haikupokelewa vizuri na benchi la ufundi, likitafsiriwa kama kwenda kinyume na utaratibu wa timu.
Kocha wa viungo alifikisha taarifa kwa Kocha Mkuu, Steve Barker, ambaye baada ya kupokea maelezo hayo aliamua kuchukua hatua ya kumuondoa mchezaji huyo kambini ili kulinda nidhamu na utulivu wa kikosi.
Inaelezwa kuwa Barker hakutaka suala hilo livuruge maandalizi ya mchezo wa Dodoma Jiji, amesisitiza kuwa kila mchezaji anapaswa kufuata maelekezo ya timu bila ubishi.
Amewaelekeza viongozi wa klabu hiyo kukaa na mchezaji huyo kulijadili suala hilo kabla hajateua kikosi kitakachosafiri kwenda Zanzibar kwa ajili ya mchezo dhidi ya watani zao, Yanga SC.
Hatua hiyo inaonekana kuwa ni ujumbe mzito kwa wachezaji wote wa Simba kuwa nidhamu na kufuata taratibu za timu ni jambo lisiloweza kujadiliwa, kipindi hiki ambacho timu inapambana kuhakikisha inapata matokeo chanya katika mechi zake muhimu zijazo.