Habari za michezo
SIMBA KUFUNGWA TENA, YANGA WATOA SIRI
Vardo
February 27, 2026
3:01 pm
ZIKIWA zimesalia siku mbili kabla ya dimba la New Amaan Complex visiwani Zanzibar kuwaka moto kwa mchezo wa Kariakoo Derby, uongozi wa Yanga umeweka wazi mambo matatu muhimu wanayopaswa kuyazingatia wanapokutana na watani zao Simba.
Katika mchezo huo linalosubiriwa kwa hamu kubwa, Yanga watakuwa wenyeji dhidi ya Simba Jumapili, Machi Mosi, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia na presha ya pointi ilivyo kwa timu zote mbili.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kuna mambo matatu ya msingi ambayo wanapaswa kuyapa kipaumbele ili kuhakikisha wanaingia uwanjani wakiwa tayari kiakili na kimkakati.
Kamwe ameeleza kuwa rekodi ya Yanga kuifunga Simba mara sita mfululizo inaweza kuwapa presha wapinzani wao, hawatarajii kuona Simba wakikubali kirahisi kupoteza kwa mara ya saba.
Amesema wanaamini Simba wataingia uwanjani wakiwa na dhamira ya kuvunja mwendelezo huo na kusaka matokeo chanya.
Amegusia tofauti ya pointi tano zilizopo kwenye msimamo wa ligi kati ya timu hizo mbili, akieleza kuwa hali hiyo inaongeza uzito wa mchezo. Simba wanahitaji kupunguza pengo hilo, jambo litakalowafanya waje kwa nguvu kubwa zaidi.
Kamwe amekumbusha kuwa licha ya Simba kudondosha pointi katika mchezo wao wa mwisho kabla ya derby, hawakuwa wabovu bali walikosa bahati tu.
Ameonya kuwa hali hiyo inaweza kuwapa motisha ya kutaka kulipa kisasi dhidi ya Yanga, hivyo kufanya pambano hilo kuwa gumu zaidi kuliko wengi wanavyofikiria.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Yanga, wanachopaswa kufanya ni kuongeza hamasa, ari ya ushindani na mapambano kwa wachezaji wao.
Amesisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kuanzia kwa mashabiki kwa kuwapa sapoti ya nguvu na kuwataka wachezaji kupambana kwa dakika zote 90 ili kuhakikisha wanapata matokeo wanayoyahitaji.