Ali Kamwe
Yanga SC

Ali Kamwe Aipa Onyo Zito Simba SC: “Pointi 5 Ni Kama Mbili, Wafunge Mikanda!”

Vardo October 28, 2026 12:44 pm

MSEMAJI wa Yanga SC, Ali Kamwe, amewatuma salamu za kiushindani wapinzani wao wakubwa Simba SC, akisisitiza kuwa tofauti ya pointi tano iliyopo kati ya timu hizo ni ndogo mno na haijamaliza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kauli hiyo ya Ali Kamwe imekuja mara baada ya Yanga kuibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC, matokeo yaliyoidhihirishia jamii ya soka kuwa mabingwa hao watetezi wapo tayari kupambana mpaka dakika ya mwisho.

Akizungumza kwa kujiamini mara baada ya mchezo huo kumalizika, Ali Kamwe amewataka wadau na mashabiki wanaoibeza Yanga kutokana na pengo la pointi kutulia, akieleza kuwa kimahesabu na kitaalamu pointi hizo tano zinaweza kufutika wakati wowote.

“Niwaambie wanaoibeza ligi kwa tofauti ya pointi tano; hizi pointi tano kimahesabu ni pointi mbili. Sababu tatu ambazo zimetushinda sisi, wanazo wao na watatulisha,” amesema Ali Kamwe.

Ameongeza kuwa kikosi cha Yanga kimejipanga kikamilifu kukabiliana na presha ya mbio za ubingwa, huku akiwaonya wapinzani wao kujiandaa na ushindani mkali zaidi katika michezo inayofuata.

“Nataka niwaambie wafunge mikanda sawasawa. Yanga Afrika sasa inaingia kwenye vita hii ya ubingwa. Wafunge mikanda sawasawa, jasho litawatoka!” alisisitiza Ali Kamwe.

Vilevile, Ali Kamwe amewakumbusha wapinzani wao kuwa Yanga ni timu yenye uzoefu mkubwa wa kupambana katika mazingira magumu na haitakata tamaa katika kutetea taji lake la Ligi Kuu.

“Yanga ni bingwa mtetezi. Yanga inajua ya kusini, inajua ya magharibi, na inajua ya mashariki. Hakuna rangi ambayo hawataacha kuona. La sivyo, tutawapumulia hapo nyuma mpaka waone kwamba mambo ni magumu. Wape taarifa nimesema kwenu kwamba sasa mabingwa watetezi tumeshakaza mikanda vizuri chini. Moto wataanza kuuona,” alihitimisha Ali Kamwe

Ally Kamwe Afunguka Changamoto za Ndani Yanga SC Dhidi ya Mashujaa FC Kauli ya Fadlu Davids Yanga SC Yaibua Mzuka Mpya Jangwani