KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema timu ya sasa ya Wekundu wa Msimbazi inaelekea kuwa hatari zaidi baada ya ujio wa wachezaji wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili, akisisitiza kuwa kikosi hicho kinaendelea kuimarika kadri siku zinavyosonga.
Katika dirisha hilo, Simba SC ilisajili nyota kadhaa akiwemo Libasse Gueye, Ismael Olivier Toure, Djibrila Kassali, Anicet Oura na Inno Jospin Loemba ambao tayari wameanza kuonyesha kiwango kizuri na baadhi yao kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Barker amesema ujio wa wachezaji hao umeongeza ushindani ndani ya kikosi na kuifanya timu kuwa imara zaidi, akisisitiza kuwa mchango wao unaonekana wazi licha ya kuwa bado wako katika hatua za kuizoea timu na mazingira ya ligi.
“Loemba bado ni mgeni katika timu na pia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini kutokana na umoja na ushirikiano uliopo ndani ya kikosi naamini hadi mwishoni mwa msimu atakuwa ameshatoa mchango mkubwa na kusaidia kufikia malengo yetu,” amesema Barker.
Kocha huyo ameongeza kuwa kwa ubora wa kikosi walichonacho kwa sasa, anaamini Simba itaendelea kuimarika zaidi kuelekea msimu ujao na kuwa timu bora zaidi kuliko ilivyo katika msimu huu.