Home Habari za michezo SIKUGOMBEA UNAHODHA SIMBA, NILIAMINIWA RUSHINE

SIKUGOMBEA UNAHODHA SIMBA, NILIAMINIWA RUSHINE

0

NAHODHA na beki wa klabu ya Simba SC, Rushine De Reuck, ameweka wazi kuwa sababu ya umri wake pamoja na uzoefu mkubwa alionao katika soka ndiyo iliyochangia benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzake kumpa jukumu la kuiongoza timu hiyo kama nahodha.

Kauli hiyo ya De Reuck imekuja kufuatia kuwepo kwa maneno mitaani kuwa beki huyo raia wa Afrika Kusini amepewa kitambaa cha unahodha baada ya kudaiwa kupokonywa aliyekuwa nahodha, Shomari Kapombe.

Akizungumzia suala hilo, De Reuck amesema anajisikia vizuri kupewa jukumu la kuiongoza Simba SC, ingawa hakuwahi kufikiria au kutarajia kuwa siku moja angekuwa kiongozi wa timu hiyo uwanjani.

“Labda ni kwa kuzingatia umri wangu, unajua nimewazidi umri wachezaji wengi hapa pamoja na uzoefu. Mimi sikulazimisha, nilipewa na nikapokea kwa sababu ndani ya timu hii kuna wachezaji wengi wazuri na ambao wamekaa muda mrefu kama Shomari Kapombe na Clatous Chama, wote wameridhia mimi kuwa kiongozi wao,” amesema De Reuck.

De Reuck ameongeza kuwa hata aliyekuwa kocha wa Simba SC, Fadlu Davids, alipomleta ndani ya kikosi hicho alimueleza kuwa angekuwa nahodha, jambo ambalo amesema ni heshima kubwa kwake kujiunga na klabu kubwa kama Simba na kupewa jukumu la uongozi.