Home Habari za michezo MAPUMZIKO YAOKOA YANGA, HERSI AIBUKA NA MPANGO MKAKATI

MAPUMZIKO YAOKOA YANGA, HERSI AIBUKA NA MPANGO MKAKATI

0

Baada ya kupata sare tatu mfululizo, uongozi wa Yanga umeanza kuchukua hatua za haraka kurekebisha mwenendo wa timu hiyo.

Kupitia msemaji wake, Ali Kamwe, klabu hiyo imeeleza kuwa mapumziko ya kalenda ya FIFA yanatumika kufanya tathmini ya kina ya kilichojiri katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika michezo ya hivi karibuni, Yanga imelazimishwa sare na Azam FC kabla ya kusafiri hadi Arusha kukutana na TRA United, ambapo pia waligawana pointi hali kadhalika na Mtibwa Sugar . Matokeo hayo yameendelea kuongeza presha kwa mabingwa hao watetezi, huku mashabiki wakitamani kuona timu yao ikirejea kwenye makali yake ya ushindi.

Kamwe amesema wazi kuwa lengo la mapumziko haya ni kubaini mapungufu yaliyojitokeza na kuyafanyia kazi ili timu irejee ikiwa imara zaidi katika mzunguko wa pili wa ligi, benchi la ufundi lina nafasi ya kutosha kuchambua kwa undani kila idara ya timu.

Akizungumzia sare ya bao 1-1 waliyoipata hivi karibuni, Kamwe amesisitiza kuwa matokeo hayo si mabaya, bali ni sehemu ya safari ya kuelekea mafanikio,  kuwa kila pointi inayopatikana ina mchango mkubwa katika mbio za ubingwa.

Amesema kipindi hiki kinatoa fursa kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kutathmini mambo yaliyofanyika vizuri na yale yanayohitaji maboresho. “Tathmini hii itatusaidia kurejea tukiwa bora zaidi na wenye ushindani mkubwa,” amesema Kamwe.

Pamoja na ushindani mkali wa ligi msimu huu, Kamwe amepongeza kiwango kinachooneshwa na timu hiyo katika baadhi ya michezo, akibainisha kuwa bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi kadri msimu unavyoendelea.

Katika mpango mkakati unaoratibiwa na uongozi chini ya Rais wa klabu, wamejipanga kuimarisha safu ya ushambuliaji ili kuongeza ufanisi wa kufunga mabao, sambamba na kuimarisha safu ya ulinzi ili kupunguza makosa yanayoigharimu timu.

Kwa upande mwingine, uongozi umeendelea kushirikiana kwa karibu na benchi la ufundi kuhakikisha kila hatua inayochukuliwa inalenga kuifanya Yanga kuwa imara zaidi na yenye ushindani wa juu.

Kamwe amewashukuru mashabiki wa Yanga kwa sapoti yao kubwa, akiwataka waendelee kuwa pamoja na timu katika kipindi hiki cha maandalizi, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika safari ya kuelekea mafanikio.