Home Habari za michezo GAMONDI, TAIFA STARS TUPO TAYARI KUIVAA LIECHTENSTEIN

GAMONDI, TAIFA STARS TUPO TAYARI KUIVAA LIECHTENSTEIN

0

KOCHA  Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema kikosi chake kipo tayari kuanza vyema michuano ya FIFA Series kwa kuonyesha soka la kuvutia na lenye matokeo kitakaposhuka dimbani dhidi ya Liechtenstein leo nchini Rwanda.

Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo huo wa kimataifa saa 11:30 jioni, huku pambano la ufunguzi wa michuano hiyo likipigwa saa 8:30 mchana. Mchezo huo unatazamwa kuwa kipimo muhimu kwa timu hiyo katika maandalizi yake ya mashindano ya kimataifa.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Gamondi amesema benchi la ufundi limeendelea kuboresha maeneo ya kiufundi na kimkakati ili kuhakikisha timu inaingia uwanjani ikiwa na mfumo sahihi kulingana na aina ya mpinzani.

Ameeleza kuwa lengo kuu ni kuijenga Taifa Stars katika mfumo imara wa uchezaji utakaowezesha timu kucheza kwa ubora huku ikiongeza nafasi ya kupata ushindi.

“Tunafanya kazi ya kuboresha masuala ya kiufundi na namna ya kucheza kulingana na mpinzani tuliyenaye. Lengo ni kuwa na timu inayocheza vizuri na yenye ushindani,” amesema Gamondi.

Kocha huyo pia amegusia matarajio makubwa ya mashabiki wa Tanzania, akisisitiza kuwa anaelewa hamasa waliyonayo kila timu inapokuwa kwenye majukumu ya kimataifa.

Hata hivyo, amebainisha kuwa katika soka hakuna uhakika wa matokeo, lakini ameahidi kuwa kikosi chake kitapambana kwa nguvu zote, kitaonyesha nidhamu, umakini, kujituma na ari ya ushindi ndani ya uwanja.